Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof .Adolf Mkenda akimsikiliza mmoja wa wanafunzi katika hafla hiyo iliyofanyika mkoani Arusha .
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof . Adolf Mkenda,ameitaka jamii kuhamasisha wasichana wa kike kuwekeza katika sayansi kwani idadi iliyopo ya wasichana katika masomo hayo ni ndogo sana ,hivyo juhudi zaidi zinatakiwa kufanyika kuhakikisha mwitikio unakuwa mkubwa zaidi.
Ameyasema hayo mkoani Arusha katika kuhitimisha siku ya kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake na wasichana katika Sayansi huku akisisitiza kuwekeza katika sayansi kwa kuwapatia vijana fursa ya ajira.
Aidha maadhimisho hayo yalibeba kauli mbiu ya “Wanawake na wasichana katika uongozi wa Sayansi Enzi mpya ya maendeleo Endelevu”.
Aidha Profesa Mkenda amesema ili kuendana na kasi ya Teknolojia ni lazima wazazi wajikite katika kuwawekea mazingira rafiki watoto wa kike ambayo yatawajenga katika kupenda masomo hayo.
Mkenda amesema kuwa wanawake na wasichana ni watu muhimu kwa mustakabali wa Sayansi iliyo bora ambayo hupelekea upatikanaji wa ajira ya uhakika kutokana na kubuni vitu mbalimbali vitakavyosaidia nchi katika maswala ya ubunifu.
“Tunapoteza sanaa kama nchi kutowapa nafasi wasichana wengine kwenda kusoma masomo ya sayansi unaweza kuwa mjasiriamali lakini bila sayansi na teknolojia hatuwezi kufika mbali tunatakiwa kuwekeza katika elimu ya sayansi na teknolojia kwa sababu wenzetu wamejiwekeza katika elimu hiyo.”amesema .
Hata hivyo amesema Fursa za kazi duniani tunako enda zinategemea elimu ya TEHAMA tusipoweza kuwafundisha vijana wetu katika eneo la sayansi tunawanyima fursa za ajira.
” Wizara ya elimu imejipanga vizuri kuendelea kutekeleza ufadhili kwa wahitaji wote na sisi wote na wadau wa elimu tutakuza sayansi hapa nchini na tutafanya kila liwezekanalo wasichana wengi kusoma masomo ya sayansi ili kukuza uchumi wetu”.amesema.
Akizungumza kwa niaba ya wadau wa Elimu Prof. Juma Khatibu kutoka shule ya Arusha Science amesema ni muhimu Kuhusisha elimu ya ubunifu na ajira ili kuweza kuwapa vijana wa kitanzania fursa katika miradi mbalimbali itakayofanywa nchini .
“Elimu bora ni elimu ya ubunifu na ajira ambayo itasaidia kuondoa changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa ajira Tanzania.”amesema.
Naye Jovian Mlay kutoka mtandao wa jinsia Tanzania TGNP amesema kuwa katika maendeleo endelevu eneo nyeti la sayansi umma unatakiwa kujua kufanya mjadala wa masomo ya sayansi kwa watoto wa kike kwa kushirikishwa shughuli zote katika vyuo na shule za msingi na Sekondari huku walimu wakiongeza bidii ya kufundisha kwa kutumia mbinu shirikishi ili watoto waweze kupenda somo la Hesabu.
Kwa upande wake Mwanafunzi mmoja ambaye ni mshiriki kutoka shule ya Arusha Science Rose Mziray amesema kuwa baadhi ya changamoto kubwa inayochangia kutotambulika katika elimu sayansi ni pamoja na Mila na desturi ambazo zinawakandamiza wao kutofikia malengo huku akiiomba serikali kuwazingatia wale waliopo katika mazingira magumu ya kupata elimu hiyo.
Maadhimisho hayo yanalenga kutambua mchango wa wanawake na wasichana katika Sekta hiyo na mafanikio ya Teknolojia, uhandisi na Hisabati (STEM )