Mkurugenzi kinga na elimu ya afya Dkt. Salim Slim akitoa taarifa kuhusiana na zoezi la utoaji wa chanjo kwa watoto chini ya umri wa miaka 5 litakalofanyia kuanzia febuari 15 hadi 18 mwaka huu, hafla iliyofanyika wizara ya afya Zanzibar
PICHA NA FAUZIA MUSSA- MAELEZO ZANZIBAR
Na Fauzia Mussa, Maelezo Zanzibar
Wizara ya Afya Zanzibar imesema itaunga mkono zoezi la kampeni ya chanjo ya Surua /Rubella kwa watoto wote wenye umri wa kuanzia miezi 9 hadi miaka 5 litakaloendeshwa na Wizara ya Afya Tanzania.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dkt Salim Slim amesema kuanzia Februari 15 hadi 18 mwaka huu , Wizara ya Afya ya serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania itaendesha zoezi hilo katika mikoa yake yote hivyo Zanzibar itaunga mkono kwa kuwachanja watoto waliopo Zanzibar ambao wanaishi Tanzania bara katika tarehe hizo ili kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo hiyo.
“Kwa vile zoezi la kampeni ya Chanjo ya Surua litakua linaendelea huko Tanzania Bara, watoto wote wenye umri kuanzia miezi 9 hadi miaka 5 ambao wanaishi Tanzania Bara, ila kwa kipindi hiki wapo Zanzibar, wanapaswa kupelekwa vituo vya Afya au maeneo yatakayokua yanatoa huduma za chanjo ndani ya Shehia ili kupatiwa chanjo ya Surua/Rubella” alifafanua Dkt Slim
Alifahamisha kuwa wakati kampeni ya chanjo ya surua ikindelea kufanyika Tanzania Bara, Zanzibar itaendesha zoezi la kuwapatia chanjo watoto wote walioko chini ya umri wa miaka 5 ambao hawakukamilisha ratiba za kupatiwa chanjo zinazostahiki.
“Zoezi la kuwachanja watoto waliokuwa hawakukamilisha ratiba za chanjo au kpata chanjo kabisa litafanyika sambamba na uendeshaji wa kampeni ya chanjo ya Surua/Rubella zoezi litakalofanyika Tanzania bara”. Alifahamisha Dkt. Slim
Hivyo amewaomba na kuwashauri wazazi na walezi kuhakikisha kwamba wanatumia fursa hiyo kuwapatia chanjo watoto wao ambao hawajakamilisha ratiba au hawajapata kabisa chanjo hizo.
Katika hatua nyengine amesema Zanzibar imefanikiwa kutokomeza magonjwa ya ndui, dondakoo, kifaduro, pepopunda ya watototo wachanga pamoja na kufanikiwa kuudhibiti ugonjwa wa surua na kuwa sio tishio tena kwa watoto na kusema kuwa Zanzibar imekua miongoni mwa nchi zisizo na virusi pori vya Polio vinavyosababisha ulemavu kwa watoto wadogo.
Amesema imethibitika kuwa chanjo ni mkakati muafaka katika kutokomeza maradhi na kupunguza vifo vya watoto, ambapo kwa kwa sasa Zanzibar haina mripuko wa ugonjwa wa Surua.
Itakumbukwa kwamba Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limethibitisha kuwa chanjo huzuia takribani vifo million 2 hadi 3 kila mwaka kutokana na maradhi yanayokingwa kwa chanjo duniani.