MSHAURI mwandamizi wa shughuli za utekelezaji wa Mradi wa Usaid Afya yangu RMNCAH Dkt Riziki Ponsiani alisema suala la mama kujifungua salama ni kipaumbele cha Mradi wa USAID Afya Yangu – RMNCAH.
Watendaji wa wilaya za mkoa wa Tabora na halmashauri na watoa huduma za afya ya mama na mtoto mkoani Tabora katika ukumbi wa mikutano wa mtemi Isike Mwanakiyungi
Mganga wa mkuu wa Hospitali ya Rufaa KiteteTabora Dkt Honoratha Rutatinisibwa alilipongeza shirika la Jhpiego kwa kutoa vifaa tiba hivyo ambavyo vitakwenda kusaidia huduma za mama na mtoto
Na Lucas Raphael,Tabora
Mkoa wa Tabora umepata msaada wa vifaa tiba vyenye thamani za zaidi ya milioni 45 kwa lengo la kuimarisha huduma za dharura kwa akinamama na watoto wakati wa kujifungua.
Akizungumza na wakuu wa wilaya ,wakurungezi watendaji wa halmashauri na watoa huduma za afya ya mama na mtoto mkoani Tabora katika ukumbi wa mikutano wa mtemi Isike Mwanakiyungi mshauri mwandamizi wa shughuli za utekelezaji wa Mradi wa Usaid Afya yangu RMNCAH Dkt Riziki Ponsiani alisema suala la mama kujifungua salama ni kipaumbele cha Mradi wa USAID Afya Yangu – RMNCAH.
Alisema kwamba lengo ni kuunga mkono juhudi za serikali katika mkakati wake wa kuimarisha afya ya mama na mtoto na kwa na kupunguza vifo vya mama na watoto .
Dkt Riziki alisema Vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kutoka 66 mwaka 2022 hadi 63 mwaka 2023.
Alisema kwamba Idadi ya akina mama wajawazito waliojifungulia katika vituo vya huduma wameongezeka toka 117,334 mwaka 2022 hadi 127,687 mwaka 2023.
Hata hivyo aliongeza kusema kuwa Matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango kwa ujumla yameongezeka toka 131,006 mwaka 2022 hadi 336,607 mwaka 2023.
Alisema kwamba Mradi unaendelea kuunga juhudi za serikali za kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za Afya.
Dkt Riziki alisema kwamba katika kipindi cha miaka miwili wateja 186,487 walipata huduma mbalimbali za Uzazi wa mpango kupitia huduma za mkoba zilizofadhiliwa na mradi.
Alisema mradi huo uliwezesha watoa huduma 164 kutambua na kutibu kwa usahihi magonjwa makuu yanayochangia vifo vya Watoto chini ya miaka mitano kama kuharisha, Malaria na magonjwa ya mfumo wa hewa ikiwa ni pamoja na utambuzi wa dalili za Hatari (Emergency triage and Treatment).
Dkt Riziki aliendelea kusema kuwa waliboresha huduma za matibabu kwa Watoto wachanga- ambapo watoa huduma 34 walipata mafunzo ya kuanzisha huduma za watoto wachanga (Neonatal care) na baada ya mafunzo zaidi ya vituo 16 vimeweza kutenga vyumba kwa ajili ya huduma za Watoto wachanga (njiti).
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Tabora mara baada ya kupokea msaada huo wa kimkakati , mkuu wa wilaya ya Tabora mjini, Louis Bura alisema serikali inatambua mchango wa asasi zisizokuwa za kiserikali katika kuwahudumia wananchi hivyo msaada huo umefika kwa wakati.
Alisema kwamba kupatikana kwa vifaa tiba hivyo kutasaidi kupunguza changamoto kwenye sekta ya afya mkoani hapa .
Aliwataka watoa huduma kutumia vifaa hivyo kwa lengo lililokusudiwa la kusaidia na kuboresha huduma bora za jamii za afya .
‘Natoa ushauri kwenu ili mtambuke kwa jamii katika maeneo mbalimbali watumieni wakuu wa wilaya wenu kwa sababu wao ndio viongozi ambao wanafanyakazi za wananchi ‘alisema Bura
Mganga wa mkuu wa Hospitali ya Rufaa KiteteTabora Dkt Honoratha Rutatinisibwa alilipongeza shirika la Jhpiego kwa kutoa vifaa tiba hivyo ambavyo vitakwenda kusaidia huduma za mama na mtoto kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Dkt Honoratha alisema kwamba shirika la Jhpiego limeunga mkono jitihada za serikali kwa sababu imejiwekeza katika ujenzi wa vituo vya afya na hospitali nchini
Mkoa wa tabora ni miongoni mwa mikoa 11 ya Tanzania bara na mikoa 5 ya visiwani ambayo inahudumiwa na Mradi wa USAID Afya Yangu-RMNCAH,na kufadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Tanzania, kupitia Shirika la Jhpiego Tanzania wenye lengo la kuimarisha huduma za dharula kwa akinamama wakati wa kujifungua.