Pichani wa kwanza kushoto ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Louis Chomboko
Na Albano Midelo,Songea
Mkoa wa Ruvuma unatarajia kutoa chanjo ya surua-Rubela kwa watoto zaidi ya 200,000 wenye umri wa kuanzia miezi tisa hadi miezi 59.
Kampeni ya kitaifa ya chanjo ya surua-Rubella inatarajia kufanyika nchini kote kuanzia Februari 15 hadi 18 mwaka huu.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Louis Chomboko amesema chanjo hiyo inawahusu watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano na wasiopungua miezi tisa na kwamba chanjo itafanyika katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya,shuleni na maeneo mengine yatakayoteuliwa .
Amelitaja lengo la kampeni hiyo ni kuimarisha kinga za watoto na kuikinga jamii dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo,kuzuia ulemavu na vifo. Amesisitiza kuwa chanjo hizo ni salama na zinatolewa bure hivyo ametoa rai kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo .