Na John Walter -Manyara
Ukatili wa kijinsia unasalia kuwa kitendo cha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu duniani kote.
Nchini Tanzania Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa raia wa kwanza kuonesha wazi kukerwa na wanaofanya vitendo hivyo viovu na kuagiza vyombo vinavyohusika kusimamia kikamilifu kuvitokomeza.
Ukifika mkoani Manyara ukatili unazungumzwa kila uchwao lakini bado wapo wasiosikia hali ambayo imemlazimu Kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Manyara George Katabazi kulazimika kuingia mtaani na kwenye vijiji kuzungumza na wananchi akisisitiza kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na vitendo vingine vya uhalifu kwa kutoa taarifa kabla tukio halijatokea.
Mkoa wa Manyara ni Miongoni mwa mikoa inayotajwa kuongoza kwa matukio ya ukatili vikiwemo vipigo, ubakaji na mauaji.
Februari 6 mwaka huu majira ya asubuhi katika kijiji cha Magugu, Binti (19) mwenye ulemavu wa kutokusikia na kuongea, alibakwa na mtu mmoja anayedaiwa aliwahi kuhukumiwa jela miaka 30 mwaka 2022 kwa Kosa la kumbaka Binti huyo huyo na baadaye kuachiliwa huru baada ya kukata rufaa.
Akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Magugu wilayani Babati, Katabazi amesema vitendo vya Ukatili haswa ubakaji vinavyofanyika katika kata ya Magugu na maeneo mengine ya mkoa wa Manyara sio vya kunyamaziwa kwa kuwa vinaharibu taswira ya mkoa.
Jeshi hilo limeahidi kumtafuta na kumkamata mtuhumiwa huyo ili kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria kujibu tuhuma zinazomkabili.