Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akijibu Maswali ya wabunge wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo Bungeni jijini Dodoma, Februari 8, 2024.
….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania wanaoishi katika maeneo hatarishi hususani ya mabondeni waondoke ili kupunguza maafa yanayoweza kusababisha mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha inarejesha miundombinu iliyoharibika kutokana na mvua hizo inarudishwa ili wananchi waendelee na shughuli zao.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Februari 8, 2024) wakati akijibu swali la Mbunge wa Kishapu, Mhe. Boniphace Butondo katika kipindi cha maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma. Mbunge huyo alitaka kufahamu Serikali imejipangaje kibajeti kurudisha miundombinu iliyoharibika kutokana na mvua.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka watendaji wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) wahakikishe wanafuatilia maeneo yaliyoathirika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na wafanye ukarabati wa kurejesha miundombinu iliyoharibika zikiwemo barabara na madaraja.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema dunia inaenda kwenye maendeleo makubwa ya matumizi ya mifumo ya kielektroniki na umma umeanza kuelimishwa juu ya matumizi hayo, lakini hata hivyo baadhi ya watu wamekuwa wakitumia vibaya mifumo hiyo kwa kukashifu na kudhalilisha watu wakiwemo watoto na wanawake.
“Hata juzi tulivyokuwa tunapitisha Muswada wa Vyama vya Siasa tumelizungumza hili na tumeliwekea kibano kwa wale watakaotumia vibaya mitandao kwa ajili ya kudhalilisha watu kwenye eneo la siasa. Pia Serikali imeweka mkakati wa kukabiliana na unyanyasaji, vitendo vya ukatili kwa watoto, wanawake na makundi mengine.”
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jansia, Wanawake na Makundi Maalumu imeweka utaratibu wa kukabiliana na wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kudhalilisha watu. “Serikali itaendelea kuimarisha udhibiti wa matumizi mabaya ya mitandao kwa kuwachukulia hatua kali wote watakaobainika kufanya hivyo”.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Nusrat Hanje, aliyetaka kufahamu Serikali imejipangaje kuhakikisha inatengeneza mazingira bora ya kisera na kisheria ya ulinzi wa watoto mtandaoni. Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi sahihi ya mitandao hiyo.
Awali, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Ng’wasi Kamani aliyetaka kufahamu kuwa mpango wa Serikali wa kuweka picha ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye fedha za Tanzania kwa kuwa ni Rais wa kwanza mwanamke na anafanya kazi nzuri, Waziri Mkuu alisema Serikali imepokea ushauri huo.
Waziri Mkuu aliongeza kuwa awali uwekaji wa picha za viongozi mbalimbali katika fedha ulikuwa ni uamuzi uliofanyika kwa lengo la kukumbuka mchango wa viongozi hao wa Tanzania na picha zinazotumika hivi sasa ni za Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume.
Mheshimiwa Majaliwa aliongeza kwa kusema kuwa mara nyingi uamuzi wa kuweka picha kwenye fedha hufanywa na kiongozi kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kwamba Serikali inatambua mchango mkubwa unaoendelea kufanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maendeleo ya Taifa, hivyo Serikali imepokea hoja ya mbunge huyo.