Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akifungua kikao kazi cha nne (4) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Na. Veronica Mwafisi-Arusha
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewataka watalaam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutatua changamoto wanazokutana nazo wananchi wanaotumia mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Mhe. Simbachawene ameyasema hayo leo wakati akifungua kikao kazi cha nne (4) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
“Nina furaha kubwa kwamba leo ninazungumza na watu sahihi, hivyo ni imani yangu kuwa, kwa muda huu wa siku tatu mtakaokuwa hapa mtaweza kuzungumza yale yaliyofanikiwa katika TEHAMA, mtakubaliana kwa uwazi lakini pia mtazungumzia changamoto ambazo wateja wetu wanaotumia mifumo ya TEHAMA wanakutana nazo,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.
Ameongeza kuwa, kuimarika kwa Taasisi ya eGA kunatokana na nia ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukuza matumizi ya TEHAMA katika utendaji kazi wa Serikali ili kuwezesha utoaji wa huduma kwa umma kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa urahisi popote walipo.
Amesema pamoja na yote yatakayozungumzwa katika kikao kazi hicho, kikubwa ni suala la utoaji wa huduma kwa wananchi, kipimo chake ni dhahiri kwani wananchi wakilalamika na kukaa kwenye foleni maana yake watumishi hawajatimiza wajibu wao.
Hivyo kila mmoja awajibike katika eneo lake ili kufikia azma ya dhati ya Rais. Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya utoaji wa huduma bora kwa umma kwa ustawi wa taifa.
Akimkaribisha Waziri Simbachawene kufungua kikao kazi hicho, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amesema katika kuhakikisha TEHAMA inaimarika Serikalini kama ambavyo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza mara kwa mara, Ofisi ya Rais-UTUMISHI itaendelea kuboresha miundo ya kiutumishi pamoja na stahiki za wataalam wa TEHAMA ili kuhakikisha wanatumia taaluma zao ipasavyo kuleta matokeo chanya kwa maendeleo ya taifa letu.
Amesema mafanikio ya Serikali Mtandao ni jumuishi kwa kada zote hivyo Ofisi ya Rais-UTUMISHI itaendelea kusimamia na kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa kada zote ili kufanikisha ujenzi wa Serikali ya Kidijitali.
Akielezea majukumu ya utekelezaji wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mkurugenzi Mkuu wa eGA Mhandisi Benedict Ndomba amesema Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na dhamira yake ya dhati ya kutaka kuwa na Serikali Mtandao, kupitia Ofisi ya Rais-UTUMISHI amekuwa akitenga fedha za kutosha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya TEHAMA.
Amesema zaidi ya washiriki 1,000 kutoka taasisi za umma wanashiriki kikao kazi hicho kinaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Uzingatiwaji wa Sera, Sheria, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao Kwa Ubadilishanaji Salama wa Taarifa.’
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akifungua kikao kazi cha nne (4) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Sehemu ya washiriki wa kikao kazi cha nne (4) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (hayupo pichani) wakati akifungua kikao kazi hicho katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi, akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kufungua kikao kazi cha nne (4) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) Mhandisi Benedict Ndomba akielezea majukumu ya eGA kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kufungua kikao kazi cha nne (4) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akifuatilia kikao kazi cha nne (4) cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).