Wahadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania wanalo jukumu adhimu la kuandaa matini za kufundishia na kujifunzia ili wanafunzi watumie matini hizo kujifunzia wakiwa huko huko walipo katika kazi zao, biashara zao, kilimo, uvuvi, ufugaji, mama lishe, baba lishe, machinga na shughuli mbalimbali za ujenzi wa taifa. Wanafunzi wanapaswa kusoma bila kuacha shughuli hizo tangu kuanza masomo mpaka kuhitimu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Machapisho, Utafiti na Uvumbuzi wa OUT Dkt. Harrieth Mtae kwenye ufunguzi wa warsha ya mafunzo ya uandishi wa matini za kufundishia na kujifunzia kwa wahadhiri wa OUT kuanzia Februari 06, 2024 hadi Februari 09, 2024 jijini Dodoma.
Akifungua warsha hiyo, Dkt. Mtae, alidokeza kuwa changamoto inayokikumba Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa upande wa matini za kufundishia na kujifunzia ni kwamba matini za zamani zinahitaji kufanyiwa mapitio ili kuweka maarifa mapya yaliyotokana na Mapinduzi ya teknolojia yaliyochagizwa na utandawazi.
“Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinajivunia sana kuwa na matini za kutosha za kufundishia na kujifunzia katika ngazi mbalimbali. Matini hizi zimekuwa na umuhimu mkubwa kwa wanafunzi si wa OUT pekee bali wa vyuo vikuu mbalimbali nchini na nje ya nchi. Hivyo basi mafunzo haya yamelenga kuwajengea uwezo wahadhiri ili kufanya mapitio mujarabu wa matini hizo na kuongeza maarifa mapya ,” amesema Dkt. Mtae.
Akiongea katika warsha hiyo, Mhadhiri Mkongwe wa chuo hiki, Prof. Emmanuel Babyegeya, ameshauri kuwa matini zilizopo zinaweza kupitiwa tena na kuzalishwa upya ili kuendana na mahitaji ya sasa ambapo maendeleo ya sayansi na teknolojia yameshika hatamu.
“Hakuna sababu kubwa ya kutumia fedha nyingi, muda na nguvu kuandaa vitabu vipya ilhali vitabu vilivyopo vilishakidhi mahitaji ya wakati wa nyuma hivyo vikiweza kupitiwa na kutengenezwa kama matoleo mapya bado vinaweza kukidhi mahitaji yaliyopo,” amesisitiza Prof. Babyegeya.
Aidha, Prof. Modest Varisanga, ambaye pia ni Mhadhiri wa Kitivo cha Sayansi, Teknolojia na Taaluma za Mazingira- Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, kupitia mjadala huo naye alitoa ushauri kuwa swala la kupitia vitabu vya zamani na kutoa matoleo mapya yaliyoboreshwa kuendana na wakati wa sasa liangaliwe kwa uzito kwani mpaka hivi sasa bado kuna taasisi mbalimbali zinaendelea kutumia vitabu hivyo kama sehemu za marejeo katika masomo yao na hivyo kuonesha kuwa bado vina umuhimu wake nchini.
Aliongeza kwamba kufanya mapitio ya matini ni kitu cha kawaida kwa sababu vitabu vya kufundishia na kujifunzia vya OUT hutumiwa na wanafunzi wa vyuo vingi. Ni dhahiri mchango wa chuo chetu katika kutoa wasomi bora nchini utazidi kukuwa na kunufaisha watu wengi kwa maendeleo ya nchi yetu na ulimwengu kwa jumla.
“Nataka kuwaambia kwamba, mimi nimeona wanafunzi wa vyuo vikuu vya hapa Tanzania tena wa vyuo vya Kampasi wanasoma matini za kufundishia na kujifunzia za OUT. Hivyo tunapofanya mapitio ni vizuri pia tukalifahamu hilo na kwa hakika linatuchagiza kuona umuhimu wa mafunzo haya,” amesema Prof. Varisanga.
Naye mhadhiri mwandamizi wa OUT Dkt. Proches Ngatuni amefafanua kwamba, uandishi wa matini za kufundishia na kujifunzia umepitia katika hatua mbalimbali za kuwa na matini za nakala ngumu, nakala laini zilizopakiwa kwenye CD, video za You Tube na sasa nakala laini zilizopakiwa kwenye mfumo wa ufundishaji na ujifunzaji kielekroniki (MOODLE) ambapo mwanafunzi anaweza kujisomea akiwa huko huko alipo akiendelea na kazi zake. Dkt. Ngatuni amesema,
“Mafunzo haya ni muhimu sana kwa wahadhiri kwa sababu pamoja na kuwawezesha kupata ujuzi wa kupitia matini zilizopo lakini pia wanapata maarifa na mbinu za kuandika matini mpya za kisasa ili kutoa wigo mpana wa marejeleo kwa wanafunzi katika masomo yao. Chuo kimepiga hatua kubwa sana katika kuhakikisha wanafunzi wanapata matini za kujisomea kupitia mitandao na hili la kuwa na vitini ama vitabu vya nakala ngumu ni muhimu sana na ndiyo maana tupo hapa.”
Naye Dkt. Yohana Lawi ambaye ni mratibu wa kitengo cha huduma za Ufundishaji na Ujifunzaji cha OUT ameeleza kwamba, mafunzo haya ya uandishi wa matini za kujifunzia ni muhimu sana kwa wahadhiri na baada ya kukamilika kwa kazi hii matini hizo zitapakiwa kwenye mfumo wa MOODLE na kuwawezesha wanafunzi kujisomea wakiwa popote wanaendelea na shughuli zao. Dkt. Lawi amefafanua kwamba,
“Lengo la OUT ni kuhakikisha kila mwanafunzi anapata huduma kwa njia ambayo ni muafaka kulingana na mazingira yake. Hivyo, matini hizi tunazoandika zitachapishwa katika nakala ngumu na nakala laini. Wanafunzi wapate machaguo ya kutumia nakala ngumu au laini kulingana na mazingira. Hii ni njia ambayo tunayo siku zote na sasa tunachofanya ni kuimarisha zaidi na kupata matini za kisasa ili kuendana na mabadiliko ya jamii kiuchumi, kisasa, kiutamaduni na kijamii,” amesema Dkt. Lawi.
Warsha hiyo ya mafunzo ya uandaaji matini za kufundishia na kujifunzia, iliyoandaliwa na Kurugenzi ya Machapisho, Utafiti na Uvumbuzi (DRPI) imehudhuriwa na wahadhiri wapatao 27 wa OUT kutoka vitivo, kurungezi na taasisi za OUT kuanzia Februari 06, 2024 hadi Februari 09, 2024 jijini Dodoma ambapo matarajio ni kwamba baada ya mafunzo haya kila mshiriki atakamilisha rasimu ya kwanza ya matini ya kufundishia na kujifunzia kwenye somo lake. DRPI itaendelea kuandaa mafunzo haya kwa wahadhiri wote wa OUT kwa awamu awamu ili kila mmoja apate mbinu na maarifa mapya ya kuandaa matini za kufundishia na kujifunzia.