Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Madaba wilayani Songea Sajidu Idrisa Mohamed akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani
Jengo la Halmashauri ya Madaba
Na Albano Midelo,Madaba
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma Sajidu Idrisa Mohamed amesema hadi kufikia Januari 31,2024 jumla ya wanafunzi wa awali 1691 sawa na asilimia 101.9 walikuwa wameripoti kuanza masomo.
Mohamed amesema hayo wakati anazungumza kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya pili kuanzia Oktoba hadi Disemba 2023 kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo mjini Madaba.
Amebainisha kuwa wanafunzi wa darasa la kwanza walioripoti ni wanafunzi 1684 sawa na asilimia 99 na kwamba wanafunzi waliopangiwa kuanza kidato cha kwanza katika Halmashauri hiyo wanafunzi 1254.
Hata hivyo amesema hadi kufikia Januari 31,2024, wameripoti wanafunzi 934 sawa na asilimia 74.46.
“Natoa rai kwa Madiwani na Watendaji Kata kuendelea kuwahamasisha wazazi,walezi na jamii kwa ujumla kuwapeleka shuleni Watoto wote ili wapate haki yao ya msingi ya kupata elimu’’,alisisitiza Mohamed.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Kapenjama Ndile amewatahadharisha wazazi na walezi wote ambao hawajawapeleka Watoto wao shule watachukuliwa hatua za kisheria na kwamba msako wa nyuma kwa nyumba utafanyika ili kuwapata Watoto wote wanaostahili kuwa shuleni.
Katika Mkoa wa Ruvuma hadi kufikia Januari mwaka huu walioripoti madarasa ya awali walikuwa ni asilimia 77, shule za msingi asilimia 91.1 na waliripoti kidato cha kwanza asilimia 60.9