Akizungumza katika zoezi hilo Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP. GEOFREY MSHANI amepongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kufanya utayari huo ambao unalenga kuwakumbusha na kuziweka tayari taasisi zinazohusika na huduma za dharura wakati wa majanga.
Sambamba na hayo amewaasa wananchi kufuata maelekezo yanayotolewa na mamlaka zenye dhamana wakati wa kufanya uokozi wa majeruhi waliopatwa na janga ili kuepusha madhara mengine yanayoweza kujitokeza wakati wa uokozi huo.
Katika hatua nyingine amesema Jeshi la Polisi lina dhamana ya kuhakikisha usalama wa raia na mali zao, hata hivyo ufanikishaji wa jukumu hilo unahitaji ushiriki na ridhaa ya wananchi. Hivyo amesisitiza wananchi kutoa taarifa za uhalifu au viashiria vya uhalifu pindi wanapobaini katika maeneo yao.
Nae Kaimu Meneja wa TRA, Mkoa wa Songwe DANIEL MISANA amesema zoezi hilo lililenga kupima wepesi na utekelezaji wa majukumu ya huduma za dharura ambapo amefafanua kwamba kwa kiasi kikubwa taasisi hizo zimeonesha kuitikia taarifa ya janga hilo kwa haraka licha ya kutokuwa na taarifa za awali.
Zoezi hilo limefanyika Januari 02, 2024 ambapo liliandaliwa na TRA likishirikisha Jeshi la Polisi, Jeshi la Zima Moto na Uokozi, TANESCO pamoja na Timu ya Dharura ya Hospitali ya Mbozi ambapo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hakuna madhara yaliyotokana na zoezi hilo.
Dawati la Habari Mkoa wa Songwe