Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linaendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa kuishirikisha jamii katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu kwa kufanya doria, misako na operesheni ambapo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 2 kwa tuhuma za kumficha mwanafunzi wa darasa la tatu, mkazi wa Mlowo Mkoani Songwe.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linawashikilia watu wawili mume na mke kwa tuhuma za kumficha mtoto mdogo mwenye umri wa miaka 08, mwanafunzi wa darasa la tatu, mkazi wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mlowo.
Tukio hilo lilitokea Januari 29, 2024, ni kwamba mtoto huyo akiwa anatoka shule akiongozana na mtoto mwenzake ambaye ni rafiki yake mwenye umri wa miaka 08, wote ni wanafunzi wa darasa la tatu walifika nyumbani kwa watuhumiwa ambao ni wazazi wa rafiki wa mhanga na hatimaye mtoto huyo akurudi nyumbani kwa wazazi wake mpaka alipotafutwa na taarifa kufikishwa Kituo cha Polisi Mlowo.
Kufuatia taarifa hizo, Jeshi la Polisi lilifika nyumbani kwa watuhumiwa Januari 30, 2024 na kufanya upekuzi kwenye nyumba hiyo na kufanikiwa kumpata mtoto huyo akiwa amefichwa kwenye chumba kimoja wapo cha nyumba hiyo huku akiwa amefunikwa ili asionekane.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa, mtoto huyu aliogopa kurudi nyumbani kwao akihofia kuchapwa na wazazi wake baada ya kuchelewa kurudi hivyo kufichwa na rafiki yake.
Aidha uchunguzi zaidi unaendelea kuhusiana na shauri hili baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa watafikishwa Mahakamani.
Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe ambao wanajihusisha na uhalifu, ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto kuacha mara moja kwani awatoweza kukwepa mkono wa sheria.