Na Mwandishi Wetu, Kongwa.
Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilaya ya Kongwa Emmanuel Msemwa ametoa rai kwa wananchi wa wilaya ya Kongwa pamoja na wilaya nyingine za mkoa wa Dodoma kujitokeza kwa wingi kwenye maadhimisho ya miaka 47 ya kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo kwa mkoa wa Dodoma, maadhimisho hayo yatafanyika Jumapili ya Tarehe 4 Februari, kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Kibaigwa wilayani Kongwa.
“Uongozi mzima wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Kongwa unawaalika makada, wanachama, wakereketwa, wapenzi, mashabiki, wafurukutwa na wananchi kwa ujumla kushiriki maadhimisho ya miaka 47 ya kuzaliwa CCM ambayo kimkoa yanafanyika wilayani Kongwa katika Shule ya Msingi Kibaigwa ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na Mlezi wa mkoa wa Dodoma Ndugu Leila Burhan Ngozi” amesema Msemwa.
Msemwa amesisitiza pamoja nae watakuwepo viongozi wote wa chama na serikali mkoa na wilaya zote za mkoa wa Dodoma bila kusahau wabunge, madiwani na wenyeviti wa halmashauri zote za mkoa wa Dodoma.
Ikumbukwe Chama Cha Mapinduzi kimezaliwa Tarehe 05/02/1977 ambapo kwa mwaka huu kinatimiza miaka 47 tangu kuzaliwa kwake, ambapo Kaulimbiu ya mwaka huu inasema: Miaka 47 ya CCM, Shiriki Uchaguzi kwa Uadilifu, Kazi Iendelee.