Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo na Kareem Mjata ambaye amepandikizwa uloto katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kati ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma tarehe 01 Februari, 2024. Kareem Mjata amechangiwa uroto na Ndugu yake Miriam Mjata
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipinga na Deus Mwita ambaye amelazwa katika Kitengo cha upandikizaji uroto kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kati ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma tarehe 01 Februari, 2024. Mtoto huyo amemuahidi Rais Samia kuwa atasoma kwa bidii mara baada ya kupona ugonjwa wa Selimundu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimjulia hali Laurean Kanaganwa ambaye bado hajapandikizwa uloto katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kati ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma tarehe 01 Februari, 2024
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Watoto wanaopatiwa matibabu ya ugonjwa wa Selimundu pamoja na wachangiaji wao wa uloto alipotembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, Februari 1, 2024.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Wauguzi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma mara baada ya kutembelea hospitali hiyo leo, Februari 1, 2024.
……………………………
NA: WAF, Dodoma
Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, amesema katika kuendelea kuboresha huduma za afya nchini Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha zenye thamani ya shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kutibu watoto 20 wenye ugonjwa wa Selimundu (Sickle Cell) mpaka kufikia Juni 2024.
Waziri Ummy amesema hayo Leo Februari 1, 2024 wakati wa ziara ya Rais Samia katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, ambapo aliwajulia hali watoto waliopandikizwa uroto katika Hospitali hiyo.
“Hatua hii inaonyesha dhamira ya serikali katika kuboresha huduma za afya na kuhakikisha upatikanaji wa matibabu kwa watu wenye magonjwa maalum kama ugonjwa wa Selimundu ambapo hadi kufikia sasa jumla ya watoto watatu wameshapandikizwa uroto”. Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy ameongeza kuwa jitihada za Serikali katika kusaidia makundi yenye mahitaji maalum katika jamii zinaonesha azma thabiti ya kuimarisha huduma za afya na ustawi wa wananchi kwa kutoa fedha kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa mbalimbali ambapo Serikali inaonyesha kujali na kuthamini maisha ya raia wake, hasa wale walio katika mazingira magumu ya kiafya.
Aidha, ameongeza kuwa hatua hiyo inatoa ishara ya uongozi mathubuti wa Rais Samia wa kujali na kuwajibika, ambao unazingatia mahitaji ya wananchi wake.
“Rais Samia amewezesha upatikanaji wa huduma bora za afya ikiwa ni moja ya vipaumbele vya Serikali yake katika kuleta maendeleo endelevu na ustawi wa jamii”. Amesema Waziri Ummy.