Na Gideon Gregory, Dodoma.
Maafisa usafirishaji kutoka Jiji la Dodoma wamelipongeza Shirika la AMEND Tanzania ambalo linajihusisha na masuala ya kutoa elimu kuhusu usalama barabarani kwa kutoa elimu ambayo yatawasaidia kuepukana na ajali zisizo za lazima.
Akizungumza mara baada ya kutoa elimu hiyo Balozi wa mafunzo Nuhu Toyi amesema kuwa kupitia mafunzo hayo wameweza kuwasaidia maafisa usafirishaji kuendesha vyombo vyao kwa umakini bila kusababisha ajari.
“Pongezi za dhati ziende kwa Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania hususani kitengo cha afya kinachofadhiliwa na miss Vivian kwa kutambua umuhimu wa kundi hili la vijana wa bodaboda wengi ni vijana ambao tupo kati ya umri wa miaka 25,”amesema.
Amesema kazi usafirishaji wengi wao wamekuwa wakiifanya kwa mazoea kwani hawana elimu ya usalama barabarani hivyo wameona ni vyema kuzungumza nao ili kuweza kuwasaidia.
Kwa upande wake afisa usafirishaji, Laurenti Mayowa amesema alikuwa haelewi alama za barabarani lakini kupitia mafunzo hayo wamepokea kutoka shirika la AMEND Tanzania kwani limekuja kitofauti katika kutoa mafunzo yao kwani wamefundishwa kwa nadharia pamoja na vitendo.
“Tulipata mafunzo mazuri sana kwenye swala la uendeshaji wa pikipiki lakini pia tumeweza kufundishwa namna ya kutumia barabara lakini pia namba ya kutumi vyombo vyetu, kwa kweli mafunzo yalikuwa mazuri nimejifunza mambo mengi na mazuri na kabla ya mafunzo nilikuwa sielewi kwamba barabarani nilikuwa naendesha hovyo hovyo tu na baada ya mafunzo nashukuru mpaka sasaivi nime elewa na tulikuwa wengi sana tukifundishwa awamu kwa awamu nafikiri bodaboda takriban 230 au 250 kwa Dodoma hapa na sasahivi wame elimika”, amesema Mayowa.
Sambamba na hayo ameongezea kuwa alama za barabarani ni changamoto kwa madereva wengi kati kuzing’amua, huku wakidhani ni michoro tu lakini baada ya mafunzo waliyopewa wameweza kuzielewa.
“Tulifundishwa kuna alama za onyo, alama za amri, kuna alama za maelekezo kwaio hayo yote tumefundishwa lakini pia nimefundishwa alama nyengine ambazo nilikuwa sizielewi vizuri kama alama za michoro juu ya sakafu ya barabara hizo nazo nilikuwa sizielewi nilikuwa naona tu michoro na sielewi maana yake lakini baada ya elimu nimevielewa vizuri” alisema Mayowa
Pia amewasisitiza maafisa usafirishaji kubadilika na kuwa na mahudhurio mazuri ya mafunzo yanayotolewa na shirika la AMEND Tanzania kwasababu yanafundishwa kwa vitendo pamoja na kutii sheria za barabarani.
“Tumefundishwa dereva kujihami kwaio wale ambao hawajapata mafunzo hawezi kuelewa na kutii sheria akiwa yupo barabarani na anaweza kusababisha ajari kwasababu anakuwa hana uelewa wowote na vigumu kujilinda anapotumia chombo chake”,Mayowa.
Naye afisa usafirishaji kutoka kituo cha Ndasha,Bw. Ally Rashid Ally amesema kuwa bodaboda ni ajira kama zilivyo ajira nyingine na imeteka soko kubwa la ajira kwa vijana kwenye upataji wa kipato na awali haikupewa thamani kama zilivyo biashara zingine.
Aidha Bw. Ally amesema elimu iliyotewa ni msaada mkubwa kwa maafisa usafirishaji mkoani Dodoma kwani wengi wao wamekuwa na nidhamu iwapo wanatumia vyombo vyao barabarani na changamoto za ajali na vifo vimeweza kuepukika kutokana na maarifa waliopokea kutoka kwa wakufunzi kupitia shirika la AMEND Tanzania.
Shirika la AMEND lipo chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania limeweza kutoa elimu na mafunzo kwa maafisa wasafirishaji maarufu kwa jina la bodaboda kwa malengo ya kudhibiti wigo ajari barabarani pamoja na kuwapa mafunzo mbali mbali pamoja na utumiaji wa alama za barabarani ambazo zimekuwa zikipuuzwa na maafisa wasafirishaji hao.