Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akiwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, wakikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Wizara katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, Januari 29, 2024.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akifafanua jambo kwa Mkandarasi Vikosi vya Ujenzi na Mshauri Elekezi wa mradi kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wanaotekeleza ujenzi wa jengo la Wizara katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, Januari 29, 2024.
Mtendaji Mkuu wa Vikosi vya Ujenzi Eng. Simeon Machibya, akitoa taarifa kwa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kuhusu maendeleo ya ujenzi wa jengo la Wizara ya Ujenzi katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, Januari 29, 2024.
Mshauri Elekezi wa mradi kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch. Weja Ng’olo, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kuhusu ujenzi wa jengo la Wizara ya Ujenzi katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, Januari 29, 2024.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Eng. Aisha Amour, wakiwasikiliza Wahandisi Washauri kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), wanaosimamia utekelezaji wa jengo la Wizara ya Ujenzi katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, Januari 29, 2024.
Kazi zikiendelea za ujenzi wa jengo la Wizara ya Ujenzi katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.PICHA NA WUU
……..
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuagiza Mkandarasi Vikosi vya Ujenzi kuongeza kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa jengo la Wizara linalojengwa katika Ofisi za Serikali Mtumba, jijini Dodoma ili kuendana na ratiba ya ukamilishaji.
Bashungwa ametoa agizo Januari 29, 2024 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo ambalo hivi sasa limefikia asilimia 71 na kusisitiza ubora na viwango katika utekelezaji wake.
Bashungwa amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Mhandisi Aisha Amour, kuendelea kusimamia ujenzi huo ili kuhakikisha malengo na maelekezo ya Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa ya utekelezaji wa majengo ya Wizara katika mji huo yanafikiwa.
Aidha, amezipongeza Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi kwa ushirikiano wao walioutoa katika ujenzi huo kuanzia hatua za awali za usanifu hadi sasa ambapo Mkandarasi yupo katika hatua za mwisho za utekelezaji wa jengo hilo.
Bashungwa amemsisitiza Mkandarasi huyo kutekeleza hatua za mwisho za ujenzi vizuri (finishing) ili Ofisi hiyo kuwa ya mfano, sambamba na kuwa na mkakati wa kuwapa maarifa wataalamu wa Sekta ya Ujenzi ili kuwawezesha wataalamu hao kupata ujuzi na kuweza kutekeleza kazi hizo wenyewe.
“Wataalamu ambao watafanyakazi na Mturuki katika finishing wahakikishe wanarithisha ujuzi na utaalamu kwa Watanzania, ili kutumia wataalamu wetu katika majengo mengine”, amesema Bashungwa.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Vikosi vya Ujenzi, Mhandisi Simeoni Machibya, amemhakikishia Waziri huyo kuwa ujenzi wa jengo hilo utazingatia viwango na ubora ili kufikia malengo ya Serikali.
Mhandisi Machibya ameeleza kuwa asilimia 68 ya vifaa vitakavyofungwa katika jengo hilo vimetoka nchini kupitia makampuni mbalimbali.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi