Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameungana na wananchi wa makundi mbalimbali kupanda miti 4720 inayotarajiwa ikiwemo miti 120 ya matunda.
Miti hiyo imepandwa katika eneo la Donge Muwanda jimbo la Tumbatu lenye ukubwa wa ekari 35.7 ikiwa ni maadhimisho ya kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa.
Aidha, Rais Samia amesema siku hii inaadhimishwa kwa kupanda miti kwasababu ya kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira nchini hasa visiwani Zanzibar.
Rais Samia amesema upandaji wa miti kwa wingi pamoja na mikoko kutasaidia kurudisha hali asilia ya bahari na kupunguza kasi ya mmomonyoko wa ardhi.
Rais Samia ametoa wito kwa wananchi wa eneo hilo kuitunza miti hiyo ili imee na kuwa na manufaa kwa vizazi vijavyo.
Rais Samia ameitaka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar kuzuia uchimbaji wa mchanga kiholela pamoja na kusitisha shughuli za kukata matofali ya miamba na kutoa vibali vya uchimbaji kwa wananchi wanaokaa maeneo ya juu tu.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amezungumza kwa njia ya simu na Mkuu wa mkoa wa Njombe Mhe. Antony Mtaka, na kuwataka viongozi wa mkoa huo kuendelea kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa lishe bora kwa watoto ili wakue vizuri.