Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia nidhamu, haki, weledi na uadilifu ili kutimiza wajibu wa kulinda raia na mali zao kwa lengo la kupunguza uhalifu katika jamii.
Kauli hiyo imetolewa Januari 27, 2024 na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe ACP GALLUS HYERA katika maadhimisho ya siku maalum ya familia ya Polisi (Police Family Day) Mkoa wa Songwe yaliyofanyika katika uwanja wa michezo wa CCM Vwawa wilayani Mbozi.
ACP Hyera amesema kuwa Polisi wameapa kuitumikia Jamii ikiwezekana wapo tayari kufa kwa ajili ya kuihudumia jamii hivyo hawapo tayari kufanya kazi na Polisi wasio waadilifu.
Aidha amewataka Polisi wa kike kufuata kanuni na taratibu za kazi ya Polisi katika suala la kupata wenza wao pindi wanapotaka kuolewa ili kuepuka kuingia katika makosa mbalimbali yanayohusu uhalifu pindi watakapopata wenza wasio waadilifu.
“Ameongeza kwa kusema endapo Polisi akiolewa na mume ambaye ni mhalifu na ikabainika basi nae atakuwa amejiingiza kwenye matatizo hayo ya uhalifu.
Sambamba na hayo ACP Hyera amesema kuwa familia zao zimekuwa nguzo kubwa katika kuwasaidia Polisi hao kuondokana na msongo wa mawazo unaotokana na ugumu wa kazi walionayo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa kuzingatia nidhamu na weledi.