Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ametoa siku 30 kwa Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha wanafanyia kazi dosari na mapungufu yote yaliyopo kwenye mashine umba (transfoma) zenye kasoro ili kuendelea kutoa huduma ya umeme wa uhakika nchini.
Naibu Waziri Kapinga ametoa agizo hilo leo Januari 26 jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa upanuzi wa Kituo cha kupoza umeme cha Mbagala pamoja na njia ya msongo wa Kilovoti 132 kutoka Kituo cha kupoza umeme cha Ilala kwenda Kurasini kwa kutumia waya zinazopita ardhini.
“TANESCO nawapa siku 30 muhakikishe mnafanya marekebisho ya miundombinu ya umeme zikiwemo mashine umba kwa kuzifungia vifaa vinavyostahili ili wananchi wapate umeme wa uhakika bila kukatikakatika ovyo katika baadhi ya maeneo hapa nchini.
Haiwezekani Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anahaingaika usiku na mchana kutafuta fedha za kuwaletea maendeleo wananchi halafu tunashindwa kununua kifaa cha laki5 kwenye transfoma tuliyonunua kwa zaidi ya milioni 10. Hii sio sawa kabisa,” amesema Kapinga.
Naibu Waziri Kapinga ameongeza kuwa ni muda sasa kwa watendaji wa TANESCO kubadilika na kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia taaluma zao ili waendelee kulinda miundombinu ya umeme ambayo serikali inawekeza fedha nyingi kwa lengo la kufikisha huduma bora ya umeme kwa wananchi.
Naibu Waziri huyo amesema wataalam wa TANESCO wahakikishe wanafikisha vifaa vyenye ubora kila mahali ili mafundi wanapofika katika maeneo hayo kuvifunga wavikute vikiwa kwenye hali ya ubora.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TANESCO Kanda ya Mashariki, Mhandisi Kenneth Boymanda amesema kuwa wamepokea maelekezo hayo ya Naibu Waziri na kuahidi kuyafanyia kazi kwa haraka kuhakikisha wanaendelea kuboresha miundombinu ya umeme nchini.