NA VICTOR MASANGU,KIMARA
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) Ndugu Kiula Kingu ametembelea na kukagua miundombinu ya maji iliyoathirika na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali mkoani Dar es salaam na kuahidi maboresho yanafanyika usiku na mchana ili kurudisha huduma maeneo yaliyoathirika.
Ndugu Kiula ametembelea eneo la Kimara Michungwani darajani ambapo ambapo uharibifu umetokea kwenye bomba la inchi 6, eneo la Bonyokwa Kijiweni uharibifu umetokea kwenye bomba la inchi 8, eneo la Mbezi Magufuli uharibifu umetokea kwenye bomba la inchi 6 na eneo la daraja la Gwajima – Mivumoni uharibifu umetokea kwenye bomba la inchi 6 na kupelekea wakazi wa maeneo hayo kukosa huduma.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Ndugu Kingu amesema athari iliyotokea kwenye miundombinu ni kubwa na kupelekea baadhi ya maeneo kukosa huduma, lakini DAWASA ipo kazini kuhakikisha huduma inaimarika.
” Ni kweli tumepata changamoto ya miundombinu ya maji lakini kwa jukumu tuliopewa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma, hivyo niwaombe radhi wakazi wa Dar es salaam pia niwatoe hofu ya kuwa DAWASA tupo kazini kuhakikisha huduma inarejea na kila eneo lililoathirika linafikiwa na kufanyiwa maboresho” amesema Ndugu Kingu
Vilevile, kwa upande wa miundombinu ya majitaka ameelezea kazi bado inaendelea ya kuzibua maeneo ambayo yalipata changamoto ya kuziba baada ya kuingiwa na mchanga pamoja na taka ngumu.
” Kwa upande wa miundombinu ya majitaka mafundi wetu wapo kazini ambapo wana vifaa vya kisasa wanaendelea na kazi ya kuzibua miundombinu, tunaendela kuwaomba wananchi kuwa wavumilivu DAWASA tumejipanga kuhakikisha hali inaimarika” amesema Ndugu Kiula