Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) anayefanya kazi katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) Kelvin Mutta na Afisa muuguzi wa hospitali ya Taifa ya Moyo ya Zambia Grivas Pharaoh
wakimuhudumia mtoto aliyefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalumu ya matibabu inayofanyika nchini Zambia. Kambi hiyo ya upasuaji imewezeshwa na Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) anayefanya kazi katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) Kelvin Mutta na Afisa muuguzi wa Taasisi hiyo Mohamed Wamara wakimuhudumia mtoto
aliyefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi maalumu ya matibabu inayofanyika katika Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia. Kambi hiyo ya upasuaji imewezeshwa na Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la
nchini Israel.
Afisa muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) anayefanya kazi katika chumba cha upasuaji wa moyo Fredy Tupa akiwaelekeza wenzake wa hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia namna ya kuandaa vifaa vyakufanyia
upasuaji wakati wa kambi maalumu ya upasuaji wa moyo inayofanyika nchini Zambia. Kambi hiyo ya upasuaji imewezeshwa na Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel.
Picha na JKCI
Na Mwandishi Maalumu – Lusaka
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia wataendelea kushirikiana katika mafunzo, kufanya tafiti na kambi za uchunguzi na upasuaji wa moyo.
Hayo yamesemwa jana na Dkt. Agness Mtaja wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu kambi maalumu ya upasuaji wa moyo kwa watoto inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa hospitali ya Taifa ya Moyo ya Zambia.
Dkt.Agness ambaye ni Mkuu wa huduma za Afya katika Hospitali hiyo alisema kabla ya kuanza kwa ushirikiano huo mwaka 2022 walikwenda JKCI kujifunza na kuona huduma za matibabu ya moyo wanazozitoa ndipo mwaka jana wakasaini makubaliano ya kushirikiana ili wananchi wa Zambia wapate huduma za matibabu ya moyo katika nchi zao za Afrika.
“Nchi za Zambia na Tanzania zinahistoria kwani tunashirikiana katika mambo mbalimbali ikiwemo bomba la mafuta la TAZAMA na usafri wa reli ya TAZARA na hivi sasa tunashirikiana kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto na mafunzo kwa wataalamu wetu wa afya. Ushirikiano huu ni mzuri kwani nchi ya Afrika inaisaidia nchi nyingine ya Afrika katika kutoa huduma za matibabu ya moyo”.
“Mwaka jana tuliwapeleka wauguzi watatu JKCI kwenda kujifunza jinsi ya kuwahudumia wagonjwa mahututi na wa dharura ambao wameshamaliza masomo yao na wamesharudi nchini na katika kambi hii wanashirikiana na wenzao wa JKCI kuhudumia watoto waliofanyiwa upasuaji”,alisema Dkt. Agness.
Dkt.Agness alisema mwaka huu watawapaleka wataalamu tisa ambao ni madaktari wa upasuaji wa moyo, mitambo, usingizi na wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu, wauguzi na wataalamu wa kuendesha mashine ya kuusaidia moyo na mapafu kufanya kazi kwenda kujifunza zaidi kwani Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete imeendelea zaidi katika upasuaji wa aina mbalimbali wa moyo ukilinganisha na Hospitali hiyo yaTaifa ya Moyo ya Zambia.
“Tunaishukuru Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwatuma wataalamu hawa katika Hospitali yetu ambao tunashirikiana kufanya upasuaji na kuokoa maisha ya watoto wenye matatizo ya moyo”, alishukuru Dkt. Agness.
Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Godwin Sharau alisema kambi hiyo ya upasuaji wa moyo inakwenda sambamba na kuwajengea uwezo wataalamu wa hospitali hiyo wa jinsi ya kufanya upasuaji pamoja na kuwahudumia wagonjwa hao.
“Tumekuja na timu ya wataalamu tisa iliyokamilika katika upasuaji wa moyo kila mtaalamu anatoa mafunzo kwa wataalamu wenzake wa hapa hii itasaidia hata pale tutakapoondoka wataendelea kutoa huduma iliyokamilika kwa wagonjwa”.
“Kambi hii ilianza kwa kufanya uchunguzi kwa watoto 15 ili kubaini ni watoto wangapi wanatakiwa kufanyiwa upasuaji baada ya uchunguzi waligundulika watoto 10 ndiyo wanahitaji huduma ya upasuaji”.
“Leo (jana) ni siku ya pili tangu tumeanza kufanya upasuaji na tumeshawafanyia watoto wanne ambao wanaendelea vizuri ninaamini hadi siku ya jumapili tutakuwa tumefanya upasuaji kwa watoto saba au nane na watoto wengine watakaobaki watafanyiwa upasuaji na wenzetu hawa wa Zambia”, alisema Dkt Sharau.
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Hospitali ya Taifa ya Moyo ya Zambia Mudaniso Ziwa alisema matatizo ya moyo yako ya aina mbili kuna ya kuzaliwa nayo na mengine mgonjwa anayapata ukubwani hii ni kutokana na mtindo mbaya wa maisha watu wanaoishi hii ikiwa ni pamoja na kutokufanya mazoezi, kutokula vyakula bora, uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe uliokithiri.
“Kuna watoto wengi wanazaliwa na matatizo ya moyo ambayo ni matundu, valvu na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio wake. Ni vizuri watoto hawa wakapata matibabu hapa nchini na wasiende kutibiwa nje ya nchi labda kwa upasuaji unaohitaji utaalamu wa hali ya juu ambao sisi hatuwezi kuufanya”.
“Ninawashukuru wataalamu wa JKCI ambao wamekuja hapa kwetu na tunafanya nao upasuaji ninaamini ushirikiano huu utakuwa endelevu kwani utatusaidia na sisi tuweze kufika hatua ambayo wao wamefikia na kuweza kuokoa maisha ya watoto wetu wenye matatizo ya moyo”, alisema Dkt. Ziwa.
Nao wauguzi watatu ambao walipata mafunzo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa mahututi na dharura katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) walishukuru kwa mafunzo waliyoyapata na kusema kuwa yamewajengea uwezo wa kuwahudumia wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa moyo.
“Mafunzo niliyoyapata JKCI yananisaidia kuweza kuwahudumia wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa moyo kwani wagonjwa hawa wakiwa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) wanahitaji kupata huduma ya ziada, ninawaomba na wauguzi wenzangu waweze kuhudhuria mafunzo haya kwani yatawasaidia katika utendaji wao wa kazi za kila siku”, alishukuru Grivas Pharaoh.
Kufanyika kwa kambi hii ya upasuaji wa moyo ni utekelezaji wa mkataba wa miaka mitatu wa makubaliano baina ya JKCI na Hospitali ya Taifa ya Moyo ya Zambia wa kutibu wagonjwa, kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa Hospitali hiyo wa jinsi ya kuwatibu wagonjwa wa moyo ambao ulisainiwa tarehe 20/04/2023 jijini Dar es Salaam.
Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH la nchini Israel ndilo lililowezesha kusainiwa kwa mkataba huo pamoja na kufanyika kwa kambi hiyo ya upasuaji wa moyo kwa watoto nchini Zambia kwa kutoa vifaa tiba na kuwasafirisha wataalamu wa JKCI.