Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Parvina Kazaula akimpima jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph – ECHO) mtoto mwenye tundu kwenye moyo wakati wa kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora – KITETE.
Afisa Uuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora – KITETE Backford John akimpima wingi wa sukari mwilini mwananchi wa mkoa wa Tabora aliyefika katika Hospitali hiyo kwaajili ya kupima moyo wakati wa kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba inayofanywa na wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Picha na: JKCI
Na: Mwandishi maalumu
Wananchi wa Mkoa wa Tabora wameiomba serikali kufikisha huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo mara kwa mara katika mkoa huo kurahisisha upatikanaji wa matibabu kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na wananchi mbalimbali waliofika katika kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo ijulikanayo kama Mhe. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba inayotolewa na wataalamu wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tabora – KITETE.
Akizungumza mara baada ya kupata matibabu Samweli Masanja mkazi wa Tabora alisema amekuwa akisumbuliwa na shinikizo la juu la damu kwa muda mrefu lililompelekea kupata kiharusi.
“Nimefurahi leo nimeonana na madaktari bingwa wa moyo waliotumia muda wao kunifanyia uchunguzi wa moyo wangu na kunianzishia dawa, naiomba Serikali itusaidie wananchi tuwe tunapata huduma kama hizi mara kwa mara”, alisema Samweli
Samweli alisema hakuwahi kupima moyo lakini kwasababu aliambiwa tatizo la shinikizo la damu alilonalo linaweza kumsababishia kupata maradhi ya moyo ndio maana akatumia ujio wa wataalamu wa afya kutoka JKCI kupima moyo wake.
Mwanaidi Ramadhani ambaye ni mkazi wa Geita aliishukuru Serikali kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kufikisha huduma za kibingwa kwa wananchi wa Tabora na mikoa ya jirani na kuiomba Serikali kuwasambaza mabingwa wa magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo katika hospitali za Rufaa za mikoa ili wananchi wapate huduma kirahisi.
“Katika Hospitali zetu za Rufaa tungekuwa na madaktri bingwa wa moyo ingetusaidia kupata huduma wakati wowote mgonjwa anapohitaji huduma hivyo kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kucheleweshwa kwa huduma”, alisema Mwanaidi
Naye mzazi ambaye mtoto wake amezaliwa akiwa na tundu kwenye moyo Grace Baltazali aliwashukuru wataalamu wa afya wa JKCI kwa kumuondolea hofu baada ya kumchunguza mtoto wake na kuona tundu alilokuwa nalo mwanaye limefunga na kubaki kwa kiasi kidogo.
“Nimefurahi mtoto wangu amefanyiwa kipimo na kuonekana tundu alilokuwa nalo limefunga na kubaki kidogo, nilikuwa naishi kwa hofu kutokana na tatizo alilokuwa nalo mwanangu”, alisema Grace
Grace alisema mara baada ya kumpata mtoto wake na kuambiwa kuwa ana matatizo ya moyo alimpeleka mtoto katika Hospitali ya Rufaa Bugando ambapo alipatiwa matibabu na sasa amefanyiwa uchunguzi tena katika kambi maalumu inayofanywa na wataalamu wa afya wa JKCI.