Na Rashid Nchimbi-Arusha
Watoto wa Jamii ya Kimasai ambao ni wanafunzi wa shule ya msingi Selela iliyopo kata ya Selela wilaya ya Monduli mkoani Arusha wametakiwa kuzingatia masomo wanayofundishwa shuleni kwao.
Elimu hiyo imetolewa na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Omari Magembe ambaye ni Mkaguzi wa kata ya Majengo baada kutembelea kata jirani iliyopo chini ya Mkaguzi Msaidizi mwenzake Juma Mahega.
Mkaguzi Magembe alitoa elimu hiyo wiki ya kwanza baada ya shule kufunguliwa na aliwataka wanafunzi hao kuzingatia masomo kwani yatawaonyesha njia ya maisha yao hapo baadae.
Alisema kitendo cha kuwa na elimu kichwani ni hazina hata kama mtu hajaajiriwa serikalini au kwa mtu binafsi.
Mbali na hilo aliwataka watoto hao kutoa taarifa za matukio ya Ukatili pindi yanapowatokea wao, ndugu au marafiki zao.
Aidha Mkaguzi huyo wa Polisi aliwatajia baadhi ya watu sahihi wa kuwapa taarifa za Ukatili ikiwa ni pamoja na wazazi, viongozi wa kijiji, walimu na Polisi.
Hata hivyo Wakaguzi hao wameahidi kushirikiana na wadau werevu ili waweze kutoa msaada wa sare na vifaa vya kujifunza kwa baadhi ya wanafunzi watakaokuwa na changamoto shuleni hapo.