Na Rashid Nchimbi wa Arusha
Jeshi la Polisi wilaya ya Monduli mkoani Arusha kupitia Wakaguzi wa Kata, limeendelea kutoa elimu ya nyumba kwa nyumba dhidi ya vitendo vya uhalifu.
Hatua hiyo ni moja ya kampeni ya kuziwezesha familia hasa Watoto kuanza kuufahamu uhalifu na namna ya kukabiliana nao mapema.
Miongoni mwa wanaondelea kutoa elimu hiyo ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Juma Mahega toka kata ya Selela tarafa ya Manyara wilayani Monduli ambapo ametoa elimu hiyo katika kaya kadhaa zilizopo katika kijiji cha Selela.
Baadhi ya Wananchi na viongozi wa kijiji hicho wamesema kwamba, hatua hiyo itasaidia kujenga kizazi kitakachochukia uhalifu siku za usoni hali ambayo itasaidia kuimarika kwa usalama kijijini hapo.
Akizungumza kwa njia ya simu na Mwandishi wa habari hii, Mtendaji wa kijiji cha Selela Bi. Neema Daud amesema kwamba, kitendo cha kuwaelimisha watoto kinachofanywa na Jeshi la Polisi kupitia Mkaguzi huyo kitaleta tija hapo baadae.
“Amekuwa ni mtu mwenye ushirikiano mkubwa kati yetu na wananchi lakini pia kampeni hizi za kutoa elimu kwa jamii zimeshaanza kuleta mabadiliko baada ya vijana wengi kuanza kushirikiana vema na jeshi la Polisi na mamlaka nyingine za kiusalama”. Alisema Mtendaji huyo.
Naye Bi.Neema Mollel ambaye ni mkazi wa kijiji hicho, amekiri kupungua kwa matukio ya uhalifu kwa kiasi kikubwa tangu Mkaguzi huyo kuwepo kwenye kata hiyo na kuongeza kwa kusema kwamba, wamesherehekea sikukuu za Krismas na mwaka mpya kwa amani kabisa tofauti na miaka ya nyuma ambapo kulikuwa na matukio ya ugomvi hasa kwa vijana.