Baadhi ya wakulima wa zao la tumbaku katika kijiji cha Libango wilayani Namtumbo wakikagua maendeleo ya zao hilo katika moja ya shamba la mkulima wa kijiji hicho Abubakari Idd wa tatu kushoto.
Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa Tumbaku nchini Onesmo Mahundi,akielezea mikakati ya uzalishaji wa zao hilo kwa mwaka 2023/2024 hapa nchini.
Meneja Mkuu wa chama kikuu cha ushirika cha Namtumbo-Songea(Sonamcu)mkoani Ruvuma Juma Mwanga akizungumza na Waandishi wa Habari(hawapo pichani) kuhusu mkakati wa kilimo cha Tumbaku katika mkoa wa Ruvuma.
Na Mwandishi wetu-Songea
CHAMA kikuu cha ushirika wilaya ya Namtumbo na Songea(Sonamcu) katika mkoa wa Ruvuma,kimetenga zaidi ya Sh.bilioni 1 zitakazotolewa kama mikopo kwa wakulima wanaojihusisha na kilimo cha zao la Tumbaku mkoani humo.
Fedha hizo zimetumika kuwasaidia wakulima kujenga mabani ya kukaushia tumbaku ,kununua pembejeo na mahitaji mengine ya zao hilo kama mkakati wa Sonamcu wa kuzalisha tani 5,200 katika msimu wa kilimo 2023/2024.
Hayo yamesemwa jana na meneja mkuu wa Sonamcu Juma Mwanga,wakati akieleza maandalizi ya uzalishaji wa zao hilo kwa msimu wa kilimo 2023/2024 ulioanza tangu mwezi Disemba mwaka jana.
Alisema,msimu wa 2023/2024 Chama kikuu kimeingia mkataba na makampuni mawili yanayohitaji kununua tumbaku tani 5,300, hivyo watahakikisha wanawasaidia wakulima mikopo ya pembejeo na fedha kwa ajili kujenga mabani ili waweze kufikia malengo ya uzalishaji.
Mwanga,amewataka wakulima wa zao hilo kuhakikisha wanapanua mashamba yao na kuongeza uzalishaji katika msimu ili waweze kunufaika na uwepo wa soko la uhakika na bei nzuri kutoka kwa wanunuzi.
Alisema,katika msimu 2022/2023 Chama Kikuu(Sonamcu)kiliingia mkataba na makampuni 3 yaliyohitaji kununua tani 9,200 lakini baada ya kufanya utafiti walibaini wakulima walijiandaa kulima tani 5,200.
Lakini kwa bahati mbaya,tumbaku iliyonunua ni tani 2,300 zenye thamani ya Dola milioni 4.337,000 sawa na zaidi ya Sh.bilioni 10 huku tani 2,700 zimepotea zikiwa shambani kwa kukosa ubora unaotakiwa baada ya wakulima kushindwa kukausha.
Ametaja sababu nyingine ya kutofikia malengo ni wanunuzi kuhitaji tumbaku ya mvuke na hewa ambazo ni ngeni kwa wakulima,badala ya tumbaku ya moshi iliyozoeleka na wakulima ambayo ilianza kulimwa katika mkoa wa Ruvuma tangu mwaka 1933.
Hata hivyo alieleza kuwa,wakulima walilima tumbaku ya mvuke lakini maandalizi yake yalikuwa hafifu licha ya Chama kuwasaidia kwa kutoa zaidi ya Sh.milioni 600 kama mkopo kwa ajili ya ujenzi wa mabani,hata hivyo baadhi ya wakulima hawakutumia mkopo huo kama ilivyokusudiwa.
Amewataka wakulima,kutumia mvua za masika zinazoendelea kunyesha kwa wingi mkoani humo kufanya maandalizi ya msimu mpya wa kilimo kwa kusafisha mashamba,na kujenga mabani mapema ili kuepuka kupata hasara kama ilivyotokea katika msimu uliopita.
Alitaja sababu zilizopelekea baadhi ya wakulima kupata hasara na kupoteza fedha nyingi ni kuuza tumbaku zikiwa mbichi kwa wafanyabiashara kwa njia ya magendo(ngoda) ambapo waliuza kwa Sh.2,000 kwa kilo moja wakati makampuni yalinunua kwa Sh.8,000.
Amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,kwa kuweka ruzuku katika pembejeo hasa mbolea zinazotumika katika uzalishaji wa zao la tumbaku,kwani imehamasisha wakulima wengi kurudi mashambani.
“mfuko mmoja wa mbolea tuliokuwa tunanunua kwa dola sabini na moja leo tunanunua kwa dola sitini na tatu,hii ni hatua kubwa kwa wakulima wetu wa zao la tumbaku”alisema Mwanga.
Kwa upande wake mjumbe wa bodi ya Tumbaku Tanzania Onesmo Mahundi alisema,katika msimu 2022/2023 Tanzania iliingia mkataba na makampuni mbalimbali ya kuzalisha tani 138,000 lakini walifanikiwa kuzalisha tani 122,000.
Mahundi ambaye pia ni Mhasibu Mkuu wa Sonamcu alisema,hayo ni mafaniko makubwa katika sekta ya tumbaku ambapo Tanzania imeshika nafasi ya pili kwa uzalishaji wa zao hilo Duniani, na katika msimu 2023/2024 malengo ni kuzalisha tani 226,000 katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Abubakar Idd mkulima wa tumbaku,ameipongeza serikali kwa kuhamasisha wananchi kujikita katika kilimo cha zao hilo na Chama kikuu cha ushirika Sonamcu kwa kusimamia uzalishaji na kutafuta soko la uhakika.
Alisema,zao la tumbaku lina faida kubwa kiuchumi iwapo mkulima atazingatia ushauri na kanuni za kilimo cha kisasa badala ya kuendelea kulima kwa mazoea.