Mwenyekiti wa Taasisi ya Majlis Al-maarif Tahir Khatib Tahir (kulia) akikabidhi vifaa vya kushajihisha uchangiaji damu ,zoezi lilifanyika Amani Complex katika kilele cha miaka 60 ya Mapinduzi.
PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR
Na Fauzia Mussa, Maelezo
Mkurugenzi mtendaji na utumishi wizara ya afya Khamis Hamad Suleiman ameihimiza jamii kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wananchi.
Akitoa shukurani mara baada ya kupokea msaada wa kushajihisha wachangiaji damu kutoka Taasisi ya Majlis Al-maarif amesema mahitaji ya damu yanaongezeka kila siku kulingana na ongezeko la majengo ya hospitali kunakopelekea jamii kuwa na mwamko wa kupata huduma za Afya hospitalini hasa mama wajawazito.
Aidha alifahamisha kuwa ongezeko la ajali limekuwa likitumia damu nyingi siku hadi siku hivyo ipo haja kwa jamii kuchangia damu mara kwa mara ili kurejesha damu hiyo kwa matumizi ya mtu mwengine.
“kuna haja ya kusahajihisha uchangiaji damu ili kukidhi mahitaji yetu kwa sasa”.
Afisa uhusiano na masoko Taasisi ya mpango wa damu salama Zanzibar Ussi Bakar Muhammed amesema katika kusherehekea miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar taasisi hiyo itaendesha zoezi la uchangiaji damu katika viwanja vya Amani complex ili kuongeza upatikanaji wa damu na kukidhi mahitaji.
Alieleza kuwa kwa siku Zanzibar inahitaji chupa za damu zisizopungua mia moja jambo ambalo halijafikiwa hivyo kuendelea kuishajihisha jamii kujitokeza kuchangia damu kwa maslahi ya Taifa.
Alisema msaada huo umekuja wakati muafaka kwani utaongeza nguvu ya ushajihishaji viwanjani hapo na kuwataka wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia zoezi la uchangiaji damu.
Nae mwenyekiti wa Taasisi ya Majlis Al-maarif Tahir Khatib Tahir ameziomba taasisi za dini, binafsi vyama na Serikali kushajihisha uchangiaji wa damu kwani mahitaji ya damu hayachagui dini wala kabila.
“kila mmoja ni muhitaji wa damu, na mahitaji hayo yanaweza kuja kwa ghafla ni vyema tukachangia na kushajihisha uchangiaji damu ili kujiwekea akiba binafsi na taifa kwa ujumla.
Taasisi ya Majlis Al-maarif ni taasisi inayojishughulisha na mambo mbalimbali ya kuisaidia jamii ambapo ilikabidhi vifaa mbalimbali vya kushajihisha uchangiaji damu ikiwemo biskuti, soda, maji na fulana kwa Benki ya damu salama ili kutumika katika zoezi la uchangiaji damu litakalofanyika katika viwanja vya Amani Complex kwenye kilele cha kutimiza miaka 60 ya Mapinduzi.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Majlis Al-maarif Tahir Khatib Tahir (kulia) akikabidhi vifaa vya kushajihisha uchangiaji damu ,zoezi lilifanyika Amani Complex katika kilele cha miaka 60 ya Mapinduzi.
PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR