Na Mathias Canal, Ushetu-Kahama
Wananchi wametakiwa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu 2024.
Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mkoani Shinyanga Mhe Emmanuel Cherehani ameyasema hayo tarehe jana wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mbika Kata ya Ushetu na Kijiji cha Ilomelo kata ya Ulowa.
Mbunge Cherehani pia amewahamasisha vijana na akina mama kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo ili kuleta mabadiliko katika jamii.
“Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan toka ameingia madarakani tumeona mambo makubwa ya kimaendeleo aliyoyafanya. Hii inaonyesha ni kwa jinsi gani akina mama walivyo na uwezo mkubwa katika uongozi. Nichukue nafasi hii kuwahamasisha mama zangu, dada zangu pamoja na vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa pindi mchakato utakapotangazwa rasmi,” amesema Mbunge Cherehani.
Mhe. Cherehani pia amewataka wananchi kuchagua viongozi wenye hofu ya Mungu na wanaotaka kuwatumikia kweli kwa kuwaletea maendeleo huku akiahidi kuendelea kushirikiana na viongozi waliopo kuhakikisha wanaendelea kuboresha maisha ya wananchi katika Jimbo hilo.