Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linaendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa kuishirikisha jamii katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu kwa kufanya doria, misako na operesheni iliyofanyika Januari 09,2024 ambapo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 11 kwa kufanya shughuli za uganga bila kuwa na kibali.
Watuhumiwa hao ni Chifu wa kabila la Kinyiha aitwaye Mwene Nzunda (44) mkazi wa kijiji cha Nambala pamoja na wenzake ambao ni Anthony Yatilinga Mapumba (65) mkazi wa Ilembo, Isambi Yasinta Mghallah (80) mkazi wa Majengo, Kostebo Ngawelo Mziho (53) mkazi wa Nambala, Tamimu Balison Mdollo (57) mkazi wa Ilembo, Biton Daimon Nzunda (64) Balozi mtaa wa Nsenya Shina namba 8 na mkazi wa Nsenya, Amos Nzunda (23) Steven Mwilenga (46) David Frank Mapumba (72) mkazi wa Ilembo, George Greyson Mghala (43) mkulima, mkazi wa mtaa wa Danida kijiji cha Ilembo na Jailos Sola (42) mkulima na mkazi wa Mbimba
Kwa melezo ya watuhumiwa hao wanasema kwamba katika kijiji hicho kuna mambo yanayofanyika yanaashiria kuwa ni yakishirikina, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linakamilisha upelelezi wa kesi hii ili watuhumiwa waweze kufufikishwa mahakamani.
Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe ni marufuku kwa mtu yoyote kufanya shughuli za uganga bila kibali ikiwa ni pamoja na kitendo cha kusafisha nyumba zinazodhaniwa kuwa na uchawi kwani kitendo hicho kinaleta chuki na udhalilishaji kwa jamii. Pia kwa mtu yoyote anapotaka kufanya kusanyiko lolote ni lazima viongozi wa sehemu husika wajulishwe.
Imetolewa na;
THEOPISTA MALLYA – ACP
Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Songwe.