Waziri wa Utalii na Mambo ya kale Simai Mohamed Said akisisitiza jambo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na Mafanikio na Changamoto katika Wizara yake Ikiwa ni Shamra shamra za miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Waziri wa Utalii na Mambo ya kale Simai Mohamed Said akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na Mafanikio na Changamoto katika Wizara yake Ikiwa ni Shamra shamra za miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Na Khadija Khamis – Maelezo
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mhe. Simai Mohamed Said amesema sekta ya utalii inachangia asilimia 29.2 ya Uchumi wa Zanzibar kutokana na ongezeko la uwekezaji katika miradi ya utalii.
Ameyasema hayo wakati wa mahojiano na Waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali ikiwa ni muendelezo wa Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema kutokana na jitihada za Serikali za kuitangaza Zanzibar kiutalii ndani na nje ya nchi kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya watalii wanaoishi nchini kutoka watalii 19,368 kwa mwaka 1985 hadi kufikia 548,503 mwaka 2022.
Vile vile amesema juhudi hizo zinakwenda sambamba na kufunguliwa kwa Jengo jipya la abiria la terminal 111 kumekuwa kichocheo kikubwa cha mashirika ya ndege ya kimataifa kutua Zanzibar na kupata fursa ya kuunganisha Zanzibar na nchi nyengine za ulaya na baadhi ya Nchi za Afrika.
Sambamba na hayo Wizara hiyo inaendelea kuwatumia Mabalozi pamoja waandishi wa habari wa Kitaifa na Kimataifa kuutangaza utalii wa Zanzibar jambo ambalo limefanikisha kupata wageni wengi nchini.
Aidha alisema Serikali inaendelea kuuboresha muenekano wa mji mkongwe katika Nyanja ya usafi pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa uegeshaji wa magari kwa lengo la kuvutia mji huo.
Aidha, Mhe Simai alisema Wizara inayafanyia kazi maelekezo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi juu ya dhana ya uwekezaji katika maeneo ya kihistoria kwa lengo la kuyarudisha katika muonekano wake wa asili.