Kaimu Mkurungezi wa halmashauri hiyo Seif Salum Seif alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake juzi Hawapo Pichani
MOJA ya majengo ya mapya ya shule ya sekondari Kakola iliyojengwa na halmashauri ya manispaa ya Tabora
Na Lucas Raphael,Tabora
SERIKALI imeipatia Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kiasi cha sh bil 41.4 kwa ajili ya utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kuboreshwa miundombinu ya elimu na afya katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurungezi wa halmashauri hiyo Seif Salum Seif alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake juzi ambapo alieleza kuwa fedha hizo zimechochea kwa kiasi kikubwa upatikanaji huduma za jamii.
Alifafanua kuwa kuboreshwa kwa miundombinu hiyo kumeleta tija kubwa ya utoaji huduma kuanzia kwa watumishi na jamii kwa ujumla, na kwa sekta ya elimu wana matarajio makubwa ya kuongezeka kiwango cha ufaulu katika shule zote.
Seif alitaja sekta zote ambazo zimefanyiwa maboresho makubwa ya utoaji huduma kuwa ni elimu, afya, barabara, maji, kilimo na utawala ambapo zimejengwa nyumba bora za watumishi na kutoa usafiri kwa watendaji ili kuwarahisishia kazi.
Aidha aliishukuru serikali kwa kuipatia halmashauri hiyo kiasi cha sh bil 6.4 kwa ajili ya uboreshaji miundombinu ya afya katika hospitali ya wilaya ikiwemo kununua vifaa tiba vya kisasa.
Alitaja baadhi ya huduma zilizoboreshwa katika hospitali hiyo kuwa ni pamoja na kujengwa wodi ya kisasa ya kujifungulia akinamama wajawazito wanaofika hapo kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo zahanati na vituo vya afya.
Aidha wamejenga jengo bora la kisasa la kutolea huduma ya x-ray na mionzi, hali iliyopunguza kero ya wananchi kufuata huduma hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Kitete.
Aliongeza kuwa baadhi ya vituo vya afya na zahanati zilizopo katika kata na vijiji mbalimbali zimefanyiwa maboresho makubwa na nyingine ziko katika hatua mbalimbali ya ujenzi ili kuwezesha wananchi kupata huduma bora za afya.
Akizungumzia miradi ya elimu alimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwapatia kiasi cha sh bil 8.2 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya, vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na nyumba za walimu ili kuboresha mazingira ya kusomea watoto.
Kwa upande wa elimu ya sekondari alisema wamepokea kiasi cha sh bil 17.7 kwa ajili ya uboreshaji miundombinu ya shule kongwe za sekondari ya Tabora wavulana, Tabora wasichana, milambo na kazima ikiwemo kujengwa shule mpya katika baadhi ya kata.