Mziga wa nyuki wa kisasa wa kikundi cha ufugaji nyuki miombo kilichopo wilayani Sikonge mkoani hapa .
Kikundi cha wafuga nyuki cha Miyombo kilichoko katika kata ya Misheni wilayani katika picha ya pamoja na Afisa Uhifadhi wa TFS-Kitengo cha Nyuki, Wilayani humo Haji Abadllah aliyevaa sare .
miziga ya nyuki ya kiasili inayotumika kwa ajili ya kufugia nyuki ipo kwenye moja ya kambi za wafugaji hao
Na Lucas Raphael,Tabora
VIKUNDI vya wafuga nyuki Wilayani Sikonge Mkoani Tabora vimeshukuru serikali ya awamu ya 6 kupitia Wakala wake wa Huduma za Misitu (TFS) kwa kuwawekea mazingira mazuri ya ufugaji nyuki katika maeneo ya misitu ya hifadhi.
Wakiongea na mwandishi wa gazeti hili ili kujionea jinsi wanavyotekeleza majukumu yao walipongeza ushirikiano mkubwa wanaopata kutoka kwa Maafisa Uhifadhi wa TFS na serikali kuwawekea mazingira mazuri.
Makamu Mwenyekiti wa Kikundi cha wafuga nyuki cha Miyombo kilichoko katika kata ya Misheni wilayani humo John Mkasiwa alisema wafuga nyuki wote kwa sasa hawana kikwazo chochote cha kufanya shughuli zao.
Alibainisha kuwa miaka ya nyuma walikuwa wanahangaika sana kupata vibali lakini sasa wamewekewa utaratibu mzuri, mtu au kikundi chochote wanapoomba hupata kibali kwa wakati na kuanza shughuli zao mara moja.
Aidha aliongeza kuwa hata wanapoingia katika misitu au mapori ya hifadhi wanapewa ushirikiano mzuri na wamekuwa sehemu ya walinzi wa misitu hiyo kwa kutoa taarifa kwa TFS punde wanapoona vitendo vya uharibifu na waharifu.
Katibu wa Kikundi Mfuga nyuki Sara Moses alisema hadi sasa kikundi chao kina wanachama 56 na kina jumla ya mizinga 2,846 ya miti na maboksi na tangu waanze kazi hiyo wamepata mafanikio makubwa sana kiuchumi.
‘Tunaipongeza sana serikali inayoongozwa na mama yetu Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fursa kwa vikundi vya wafuga nyuki kufanya shughuli zao katika misitu ya hifadhi pasipo bughudha yoyote’, amesema.
Boniface Kisamba mfuga nyuki, mkazi wa Madukani wilayani humo alisema wana kila sababu ya kumpongeza Rais Samia kwa kujali ustawi wa wananchi wake na kuruhusu vikundi vya wajasiriamali kufanya shughuli zao kwa uhuru.
Aliomba serikali kuwasaidia kupata masoko ya pamoja yatakayowawezesha kuuza mazao yao ya nyuki kwa bei nzuri, pia aliomba TFS kuwapunguzia gharama ya kuingiza vyombo vya usafiri kwenye hifadhi kwa ajili ya kubebea mazao hayo.
Afisa Uhifadhi wa TFS-Kitengo cha Nyuki, Wilayani humo Haji Abadllah alieleza kuwa zaidi vya wafuga nyuki 40,000 wameshapewa vibali vya kufanya shughuli hizo na wote walipewa elimu ya ufugaji wa kisasa na utunzaji misitu.
Alibainisha kuwa wafuga nyuki ni marafiki wa TFS ndio maana wanawapa ushirikiano, hadi sasa kuna kambi zaidi ya 2000 za wafuga nyuki katika hifadhi hizo na wote wanaendelea na shughuli zao kwa kufuata sheria na taratibu.
Abdallah alifafanua kuwa ili kuhakikisha misitu hiyo inakuwa salama wanafanya doria za mara kwa mara na vikundi vyote vinavyofanya shughuli zao katika misitu hiyo vinawasaidia kulinda pia.
‘Wafuga nyuki wote wamepewa elimu ya ufugaji wa kisasa na wamesisitizwa kutumia vifaa sahihi vya uvunaji mazao ya nyuki na kutumia vizuri misimu ya mwaka ili shughuli zao zilete tija kubwa’, amesema.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka 2 wafuga nyuki kutoka vikundi 4 vya Miyombo, Kitunda, Usunga na Kiyombo walipewa ruzuku ya kati ya sh mil 5 hadi mil 50 ili kuwainua zaidi katika shughuli zao.