Waziri wa Afya Zanzibar Mhe.Nassor Ahmed Mazrui akita utepe kuashiria uzinduzi wa barabara ya ndani ya Dimani-Sokoni-Dimani- Beach pamoja na barabara ya Kombeni -Nyamanzi zenye urefu wa kilomita 2.8 ikiwa ni shamrashamra za kutimiza miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui amesema ujenzi wa Barabara ya Kombeni, Nyamanzi na Dimani bichi, Dimani maketi na vitongoji vyake ni kichocheo Cha maendeleo na upatikanaji wa ajira kwa vijana wa maeneo hayo.
Ameyasema hayo huko Nyamazi Wilaya ya Magharibi B wakati wa uzinduzi wa Barabara hizo kufuatia shamrashamra za maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema Wananchi wamaeneo hayo muda mrefu walikuwa na malalamiko ya Barabara lakini kutengezwa kwake kutaondosha changamoto walizokuwa wakizipata hasa Wanapokuwa na Watoto, Wagonjwa na Mizigo.
Amesema maeneo hayo yamo katika maeneo yanayokua kwa uekezaji na ujenzi wa majengo ya kisasa jambo ambalo litaufanya Mji huo kuwa Mji wa pili wa Zanzibar.
“Hapa zitatokea ajia kwani mkongo wa Mawasiliano Tehama unajengwa hapa, maonesho ya biashara yapo hapa, majengo mazuri yapo hapa huu utakuwa ni Mji wa Pili na utatoa fursa za ajira kwa Vijana wengi’, amesema Mazrui”
Aidha amesema kuwa ujenzi huo ni kuyaezi Mapinduzi yaliomkomboa Mnyonge kutoka katika makucha ya Wakoloni sambamba na kuwaletea maendeleo endelevu Wananchi wake.
Nae Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Shomari Omar Shomari akisoma Ripoti ya kitaalamu amesema Barabara hiyo ina urefu wa kilomita mbili nukta nana (2.8) inajengwa kwa kiwango Cha uwekaji wa tabaka lakemikali iliochanganywa na maji, uwekaji wa tabaka mbili za lami ya kokoto (chipsi) na uwekaji watabaka la lami na rojo.
Amesema Barabara hiyo inajengwa na Kampuni ya IRIS ASER kutoka Uturuki na ujenzi wake ulianza julai 17, 2022 na kukamilika Oktoba 5, 2023 ambayo magari yanayo takiwa kupita ni magari ya tani 10 na inaaminika kudumu kwa mda wa Miaka kumi.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amesema ujenzi huo utaondoa changamoto kwa Wananchi na Waekezaji na kuwa katika Mazingira mazuri.
Gharama za Ujenzi huo imechanganywa kwenye jumla ya Mradi wote wa Ujenzi wa Barabara za ndani kilomita 275.9 ambapo gharama zake zinakisiwa kuwa ni zaidi ya Dola za kimarekani Laki Nane.