Afisa Mhifadhi Misitu-Kitengo cha Nyuki, Wilaya YA Uyui , Paul Kisumu alipokuwa akiongea na mwandishi wa gazeti hili aliyetembelea Hifadhi ya Msitu wa Uyui-Kigwa Rubuga.
Hiyo ni nyumba ya ulinzi iliyopo katika Msitu wa Uyui-Kigwa Rubuga kwa ajili ya askari kukaa kwa ajili ya Doria ya mara kwa mara
Na Lucas Raphael Tabora
WAKAZI wa Vijiji 12 vilivyoko kwenye maeneo ya Hifadhi za Misitu Wilayani Uyui Mkoani Tabora wamenufaika na agizo la serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu baada ya kuongezewa maeneo ya kuishi na kufanya shughuli za kibinadamu.
Hayo yalibainishwa jana na Afisa Mhifadhi Misitu-Kitengo cha Nyuki, Wilayani humo Paul Kisumu alipokuwa akiongea na waandishi wa habari aliyetembelea Hifadhi ya Msitu wa Uyui-Kigwa Rubuga kuona jinsi misitu hiyo inavyolindwa.
Alisema wilaya hiyo yenye wakazi 562,588 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ilikuwa na jumla ya hekta zipatazo 135 za Misitu ya Hifadhi lakini baada ya maelekezo ya serikali, hekta 36 zimemegwa na kuongezewa maeneo wananchi.
Aliongeza kuwa baada ya kumega eneo la hifadhi wameweka vigingi vya mipaka mipya ili kuwezesha wananchi kufanya shughuli zao kwa upana tofauti na hali ilivyokuwa huko nyuma, katika hili wananchi wanajivunia sana.
Kisumo alifafanua kuwa baada ya kukamilisha utaratibu huo katika hifadhi zote 3 zilizoko wilayani humo za Uyui- Kigwa Rubuga, Igombe river na Simbo wamewataka wananchi kutovamia tena hifadhi hizo na kufanya shughuli zao.
‘Tayari tumewaongezea maeneo, sasa hatuhitaji kuona mtu yeyote akivuka mipaka na kuingia eneo lililokatazwa kisheria na kufanya shughuli za kilimo, ufugaji au kuchoma mkaa, tutawachukulia hatua’, alisema.
Alitaja baadhi ya vijiji vilivyokuwa ndani ya hifadhi na sasa vimerekebishiwa mipaka na kuwa nje ya hifadhi kuwa ni Kigwa, Someri, Isenegeja, Ibelamilundi, Itobela, Misole na Lutende na vingine.
Ili kuimarisha ulinzi wa misitu hiyo alisema TFS wameanza kujenga Vituo vya Ulinzi ndani ya hifadhi na kituo cha kwanza kimejengwa katika msitu wa Uyui-Kigwa Rubuga na kimekamilika wa asilimia 100 kwa gharama ya sh mil 61.
Alifafanua kuwa kujengwa kwa kituo hicho kutawezesha askari wa uhifadhi kuishi katika maeneo hayo na kufanya doria wakati wote (usiku na mchana) ili kudhibiti vitendo vya uvamizi na wavamizi.
Kisumo alisisitiza kuwa serikali wilayani humo kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye ni Mkuu wa Wilaya, Zakaria Mwansasu na Wakala wa Huduma za Misitu wameshatoa elimu ya kutosha kwa jamii hivyo hatarajii kuona mtu yeyote akiingia ndani ya hifadhi na kufanya shughuli zake.