Na. Raymond Mtani BMH-DODOMA
Imeelezwa kuwa kuzungumza kwa njia ya simu kwa muda mrefu kinaweza kuwa chanzo mojawapo cha kupoteza usikivu.
Hayo yamesemwa na Leonard Tibihika, Mtaalamu wa Upimaji Usikivu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) katika mahojiano maalumu kuhusu huduma za uchunguzi wa Usikivu Hospitalini hapo, leo Januari 5, 2024.
“isitafsirike vibaya, si kila anayeongea na simu anahatarisha usikivu, bali yule anayetumia muda mrefu kuongea na simu, kwa sababu mgandamizo wa sauti inayoingia sikioni ukiendelea kwa muda mrefu huathiri Ngoma ya Sikio” Alisema Tibihika.
Watu wengine waliyoko katika hatari ya kupoteza usikivu ni wale wanaofanya kazi katika mazingira ya kelele, alisema Mtalaamu huyo akitolea mfano, wafanyakazi wa viwandani na wanaokesha kwenye klabu za muziki, na wale wenye shughuli katika masoko.
“changamoto anayoweza kukutana nayo mtu anayepoteza usikivu ni kutogundua mapema kuwa usikivu wake hauko katika kiwango cha kawaida, akachukua hatua kwa sababu usikivu hupungua polepole wakati mwingine hadi ambiwe na wengine” Tibihika.
Kuchelewa kugundua kuwa usikivu unapotea, au kugundua na kutochukua hatua za kuchunguzwa ili kutibiwa husababisha watu wengi kufika Hospitali wakiwa katika hatua mbaya kiasi cha kuhatarisha kupoteza usikivu kabisa.
Taarifa za Vituo vya Udhibiti na Kukinga Magonjwa (CDCs) zinadokeza kuwa, Watoto na Vijana wadogo milioni 5.2 na watu wazima milioni 26 hupoteza uwezo wa kusikia kutokana na kuwa kwenye mazingira ya kelele.
Katika moja ya tafiti kuhusu kupoteza usikivu kwa matumizi makubwa ya simu uliyobandikwa katika tovuti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), unathibitisha kuwa matumizi ya zaidi ya dakika 60 kila siku yanaweza kuathiri usikivu wa binadamu ndani ya miaka 5.
Tibihika, anatoa wito kwa watumiaji wa simu kwa muda mrefu, kuchukua hatua za kujikinga, pamoja na kuhakikisha wanafanyiwa uchunguzi wa usikivu angalau mara mbili ndani ya miezi 12.
Hospitali ya Benjamin Mkapa, ni miongoni mwa Hospitali tatu za serikali nchini zinazotoa huduma za uchunguzi wa usikivu kwa kufanya vipimo vya aina zote, asilimia kubwa ya wagonjwa wanaopoteza usikivu hubainika kuwa na tatizo la kupasuka Ngoma ya Sikio.