Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kuelekea sikukuu ya Krismas na Mwaka mpya 2024 limejipanga vizuri katika kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao kwa kuhakikisha Ulinzi na usalama katika nyumba za ibada hasa katika Misa na Ibada za mkesha ambapo kama ilivyo kawaida doria na ulinzi kwa kushirikiana na kamati za ulinzi na usalama za Makanisa na Misikiti zitafanyika.
Aidha, Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kuhakikisha ulinzi na usalama katika kumbi za starehe kwa kuhimiza kila mmiliki wa kumbi ya starehe ahakikishe anaweka walinzi binafsi, anazingatia uwezo wa kumbi yake kuingiza watu ili kuepuka mlundikano wa watu ambao unaweza kusababisha madhara.
Kwa upande wa usalama barabarani, licha ya changamoto ya miundombinu ya barabara katika Jiji la Mbeya, kutakuwepo na Askari katika maeneo yenye changamoto kubwa kama vile kuanzia Mafiati hadi Ilomba na katika maeneo ya vivuko vya watembea kwa miguu.
Rai kwa watumiaji wa barabara watakaopita maeneo tete ya mlima Iwambi na Inyala – Shamwengo kuendelea kuwa wavumilivu na kufuata utaratibu uliopo wa kupitisha magari makubwa na madogo kwa awamu ili kuepuka ajali na madhara makubwa yasitokee.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa tahadhari kwa wazazi watakaokwenda na watoto katika Fukwe kama vile Matema, Ngonga Wilaya ya Kyela na Kisiba Wilaya ya Rungwe kuwa makini kwa kuhakikisha wana kuwa waangalifu kwa watoto wao. Pia Jeshi la Polisi linawataka wamiliki wa Fukwe hizo kuweka waangalizi katika maeneo yao.
Sambamba na hilo, wazazi na walezi wanakumbushwa kuwa waangalifu kwa watoto kwa kuhakikisha katika nyumba za ibada na maeneo yenye michezo ya watoto wanaenda na watu wazima ili kuepuka kupotea na kupata madhara mengine.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu. Aidha, Jeshi la Polisi linawatakiwa wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya na Tanzania kwa ujumla Kheri ya Krismas na Mwaka Mpya 2024, tusherehekee kwa Amani na Utulivu.
Imetolewa na:
Benjamin Kuzaga – ACP
Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Mbeya