Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Ilemela kimeelekeza viongozi wake kuhakikisha inafanyika mikutano mikuu kwa ngazi ya kata na matawi ili kufafanua shughuli za maendeleo zilizotekelezwa katika maeneo yao, kusikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na kutoa fursa kwa viongozi wa ngazi hizo kuweza kuzungumza na wajumbe wao
Akizungumza wakati wa mkutano mkuu maalum wa CCM wilaya ya Ilemela uliofanyika katika ukumbi wa chuo cha maliasili Pasiansi Mbunge wa Jimbo la Ilemela MNEC Mhe Dkt Angeline Mabula amewataka viongozi wa chama hicho kutembea kifua mbele kwa kuwa Serikali yao chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan imefanya kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo
‘.. Viongozi wetu wa juu wanafanya ziara, wanasikiliza wananchi kwanini sisi wa ngazi za wilaya, kata na matawi tusifanye mikutano mikuu, tusitatue kero za wananchi ..’ Alisema
Aidha Dkt Mabula amemshukuru Rais Dkt Samia kwa fedha za miradi ya maendeleo pamoja na kuwahakikishia wananchi wa kata ya Shibula wanaokabiliwa na mgogoro wa ardhi wa uwanja wa ndege kuwa na amani na kwamba Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuutatua huku akisisitiza viongozi kuhudhuria na kuwahi katika vikao vyote vinavyoandaliwa na chama
Nae Katibu wa CCM wilaya ya Ilemela Ndugu Hasan Milanga amefafanua kuwa lengo la chama cha mapinduzi ni kuhakikisha wanashinda uchaguzi na kuunda Serikali inayotatua kero za wananchi na kwamba chama hakitamvumilia mtu yeyote anaetia hofu viongozi waliopo madarakani kiasi cha kushindwa kutimiza wajibu wao huku akiziagiza Kamati za siasa na maadili za ngazi za kata na matawi kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kuanza kampeni kabla ya muda
Kwa upande wake Katibu wa siasa na uenezi wa mkoa wa Mwanza Ndugu Prudence Sempa mbali na kuipongeza Ilemela kwa kutoa hati ya pongezi kwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza Ndugu Masanja Lushinge maarufu kwa jina la Smart aliyechaguliwa hivi karibuni amewataka viongozi wa chama hicho kwa ngazi zote kutoa Elimu Kwa wananchi juu ya Bima ya afya Kwa wote iliyoanzishwa na Serikali hivi karibuni
Mkutano mkuu maalum wa CCM wilaya ya Ilemela ulihudhuriwa na wajumbe wa kutoka matawini, kata, wilaya na mkoa wanaohusika na mkutano huo akiwemo Mwenezi wa CCM mkoa wa Mwanza, Katibu wa wazazi mkoa wa Mwanza, Katibu wa UWT mkoa wa Mwanza na wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM mkoa wanaotoka ndani ya wilaya hiyo