Tenki linaloendelea kujengwa ambalo litahudumia wakazi wa vijiji vya Ngongohele,Ngunja na Mikuyu wilayani Liwale.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Liwale Mhandisi Ruhumbika Wigolo kushoto akizungumza na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ngongohele kuhusu maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji utakaohudumia kijiji hicho na vijiji vingine vya Ngunja na Mikuyu wilayani humo.
Baadhi ya wananchi na viongozi wa serikali ya kijiji cha Ngongohele wilaya ya Liwale mkoani Lindi wakikagua maendeleo ya ujenzi wa tenki la maji linalojengwa katika kijiji hicho na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa).
Na Muhidin Amri,
Liwale
WAKAZI wa vijiji vya Ngongohele,Ngunja na Mikuyu kata ya Ngongohele wilayani Liwale,wameanza kuwa na matumaini ya kupata huduma ya maji safi na salama baada ya wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kuanza kutekeleza mradi wa maji wa Hangai Corridor utakaogharimu Sh.bilioni 1,318,000,000.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Liwale Mhandisi Ruhumbika Wigolo alisema,mradi huo ulianza kutekelezwa mwezi Machi 2023 na unatarajiwa kukamilika mwezi April 2024 na muda wa utekelezaji wake ni miezi tisa.
Ruhumbika alisema,mkandarasi amelipwa Sh.milioni 247,000 kati ya Sh.bilioni 1.3 zilizoko kwenye mkataba na kazi zinazotekelezwa ni ujenzi wa tenki la lita 300,000,tenki dogo lenye uwezo wa kukusanya lita 50,000 ujenzi wa nyumba ya mitambo na vituo vya kuchotea maji 15.
Ruhumbika ametaja kazi ambazo hazijaanza kutekelezwa ujenzi wa chanzo cha kukusanyia maji(Intake)kulaza mabomba ya kusambaza maji urefu wa kilomita 7.5 kufunga pumpu na umeme jua(Solar)kwa ajili ya kusukuma maji kutoka kwenye chanzo kwenda kwenye tenki kubwa.
Alisema ni matarajio ya Ruwasa kuwa,kazi zote zitakamilika kabla ya muda uliopangwa kutokana na kasi kubwa ya mkandarasi katika kutekeleza majukumu yake na wananchi wa vijiji hivyo wapatao zaidi ya 5,000 wataanza kupata huduma ya maji safi na salama kwenye makazi yao.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Liwale Goodluck Mlinga,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji ambayo imewezesha wananchi kuondokana na changamoto ya maji.
Mlinga alisema,kwa miaka miwili 2021/2022/2022/2023 wilaya ya Liwale imepokea wastani wa Sh.bilioni 2.5 kila mwaka kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji.
Kwa mujibu wa Mlinga,fedha hizo zimewezesha wilaya hiyo kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 50 hadi kufikia asilimia 70 na mpango uliopo ni kufikisha asilimia 80 ya wananchi watakaopata huduma ya maji safi na salama ifikapo mwaka 2025.
Dc Mlinga,amemuhakikishia Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa,fedha zote zinazopelekwa katika wilaya hiyo zitasimamiwa na zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Aidha,amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuhakikisha wanatunza miradi na miundombinu ya maji inayojengwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mkazi wa kijiji cha Ngongohele Said Kelu alisema,kwa sasa huduma ya maji safi na salama katika kijiji hicho ni kero kubwa ambapo amemuomba mkandarasi kuamilisha ujenzi wa mradi huo haraka ili waanze kupata huduma ya maji kwenye makazi yao.
Abdul Kiwanga alisema,mradi huo utakapokamilika utawaondolea kero ya kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 3 kila siku kwenda kutafuta maji yanayopatikana kwenye mabonde na mito inayozunguka kijiji hicho.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Juma Mponda alisema,wananchi wa kijiji hicho wanalazimika kuamka saa 10 na 11 alfajiri kwenda kutafuta maji kwenye mito na mara kwa mara wanakutana na wanyama wakali wakiwemo Simba na Tembo ambao ni hatari kwa maisha yao.