Kamati ya kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ya jumuiya ya wanawake wa CCM wilaya ya Ilemela imezinduliwa leo na mbunge wa jimbo hilo Mhe Dkt Angeline Mabula ikiwa ni utekelezaji wa agizo la mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan na kuungwa mkono na mwenyekiti wa UWT taifa Ndugu Mary Chatanda
Akizungumza na wajumbe wa kikao cha baraza kuu la UWT wilaya ya Ilemela katika ofisi za CCM za wilaya hiyo zilizopo kata ya Buswelu, Mgeni rasmi na mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amewataka wajumbe wa kamati hizo kwenda kutekeleza wajibu wao kikamilifu kwa kuhakikisha wanafichua vitendo vyote vya kikatili na kuchukua hatua kali dhidi ya wanaofanya vitendo hivyo ili kuunga mkono maono ya Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt Samia Suluhu Hasan alipozitaka jumuiya za CCM kupambana na vitendo vya kikatili na unyanyasaji katika jamii
‘.. Mhe Rais Dkt Samia alielekeza jumuiya zipambane na ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, Lakini hakuna aliyechukua hatua mpaka alipokuja mwenyekiti wa UWT taifa Ndugu Mary Chatanda, Amezunguka nchi nzima mikoa yote kukemea hili na yote kwa sababu tuna Rais kinara anaepinga vitendo vya kikatili na unyanyasaji na nyinyi wenyewe ni mashahidi wa hili ..’ Alisema
Aidha Dkt Mabula mbali na kuwataka wajumbe hao kuyasema mazuri yaliyofanya na Serikali amempongeza Rais Mhe Dkt Samia kwa kuanzisha wizara itakayosimamia maendeleo ya jamii na jinsia kwani itasaidia kupunguza na kuzuia vitendo vya kikatili kwa kuwa itakuwa ikisimamia masuala hayo moja kwa moja tofauti na hapo awali ambapo wizara moja ilikuwa na mambo mengi kiasi cha kutoyapa sana kipaumbele mapambano dhidi ya ukatili na unyanyasaji
Kwa upande wake mjumbe wa kikao hicho ambae pia ni katibu wa CCM wilaya ya Ilemela Ndugu Hasan Milanga amekemea vitendo vya baadhi ya viongozi kushiriki vikao vya kampeni kabla ya wakati na kwamba chama hakitavumilia viongozi wa namna hiyo huku akiwataka viongozi waliochaguliwa katika nafasi mbalimbali kuhudhuria vikao na kushiriki shughuli zote zinazowahitaji bila kuwepo visingizio vya utoro
Salome Kipondya ni mwenyekiti wa UWT wilaya ya Ilemela, Amempongeza mbunge wa jimbo hilo Mhe Dkt Angeline Mabula pamoja na kumkabidhi cheti kama ishara ya kutambua na kuthamini mchango wa mbunge huyo katika shughuli za maendeleo na kuimarisha chama na jumuiya zake huku akiwataka wanawake kuendelea kuungana mkono ili waweze kujikwamua kiuchumi na kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika Serikali
Nae katibu wa UWT wilaya ya Ilemela Bi Arafa Njechele amewataka madiwani wa viti maalum kuhakikisha wanakutana na wanawake wote wanapofanya ziara katika ngazi ya kata na matawi badala ya kuonana na wajumbe wachache ili kuzuia mianya ya rushwa na mpasuko usio na sababu katika jumuiya
Jumuiya ya UWT wilaya ya Ilemela imefanya kikao chake cha baraza la kawaida ambapo walikabidhi cheti kwa mbunge wa jimbo la Ilemela Dkt Angeline Mabula kama ishara ya kutambua mchango wa mbunge wa jimbo hilo na kisha kuzindua kamati za kampeni kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024 pamoja na kamati ya kupinga ukatili na unyanyasaji kwa ngazi ya wilaya