Baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Halmashauri Wilaya ya Kilosa Kanda ya Dumila wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi alipowatembelea kuona maendeleo ya Mafunzo ya Mifumo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa wa Morogoro.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akizungumza na baadhi ya Viongozi na Watumishi wa Halmashauri Wilaya ya Kilosa Kanda ya Dumila (hawapo pichani) alipowatembelea kuona maendeleo ya Mafunzo ya Mifumo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa wa Morogoro.
Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa Mafunzo ya Mifumo ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assesment kwa Mkoa wa Morogoro, Bw. Priscus Kiwango akimueleza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi maendeleo ya mafunzo ya mifumo hiyo.
Na. Veronica Mwafisi- Dumila
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amewaasa watumishi wa umma wa Halmashauri Wilaya ya Kilosa Kanda ya Dumila kujipima kupitia Mifumo Mipya ya PEPMIS, PIPMIS na HR Assessment kwa kujaza kazi wanazotekeleza kila siku ili mfumo uweze kutoa alama sahihi.
Amesema hayo wakati alipotembelea kanda ya kimafunzo ya Dumila kuona maendeleo ya Mafunzo ya Mifumo hiyo.
Bw. Daudi amesema kuwa, mafunzo hayo yanalenga kuwaongezea watumishi wa umma ujuzi na ari ya kutumia mifumo ya TEHAMA katika kupima utendaji kazi na utekelezaji wa shughuli mbalimbali Serikalini.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inafanya juhudi kubwa katika kusimamia na kutoa stahiki na maslahi mbalimbali kwa watumishi wa umma. Hivyo, ni jukumu la watumishi kumuunga mkono kwa kutoa huduma bora kwa umma” alisema Bw. Daudi.
Aidha, Bw. Daudi ameongeza kuwa, moja ya majukumu ya Ofisi ya Rais -UTUMISHI ni kusimamia utumishi wa umma, ndio maana Serikali imebuni mifumo hiyo ambayo itaboresha utendaji kazi Serikalini kwa kumpima mtumishi mmoja mmoja na taasisi.
Bw. Daudi amefafanua kuwa kupitia mfumo wa PEPMIS kila Mwajiri atakuwa na uwezo wa kuona namna watumishi wake wanavyofanya kazi kila siku.
Naibu Katibu Mkuu huyo, amesema amefurahishwa na namna watumishi wa umma katika mkoa wa Morogoro walivyoitikia wito wa kushiriki mafunzo hayo na wameonesha utayari wa kutumia mifumo hiyo ili kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anayetaka kuona kunakuwa na utumishi wa umma bora na wenye kuhudumia wananchi kwa ufanisi mkubwa.