Na WMJJWM, Mtwara.
Wananchi wa Mkoa wa Mtwara wameipongeza Serikali kwa kuyasimamia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) na kuhakikisha yanatekeleza majukumu yake kwa jamii.
Hayo yamebainishwa wakati wa ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na NGOs unaofanywa na wataalam kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum mkoani Mtwara, Desemba 19, 2023.
Fatuma Rajab ambaye ni mnufaika wa mradi wa “Mwanamke na Uongozi” amesema mradi huo umewasaidia wanawake kwa kuwajengea uwezo wa kujiamini na kushiriki katika fursa za uongozi tofauti na mwanzo.
“Kabla ya kushirikishwa katika mradi huu wa “ Mwanamke na Uongozi” nilikua na dhana potofu kwamba mambo ya siasa na uongozi ni kwa ajili ya wanaume tu lakini hali kwa sasa ni tofauti…
nafikiria kugombea Udiwani mwaka 2025 na baadaye nafasi ya ubunge “Amesema Fatuma.
Kwa upande wake kijana Musa Turitote amesema kupitia mradi wa“ Kijana kwanza” Vijana wengi wameshirikishwa katika shughuli za kijamii ikiwemo kukemea na kupinga ukatili katika jamii pamoja na utunzaji wa mazingira.
“Viwango vya ukatili hasa kwenye jamii yetu vimepungua hususani sehemu zinazotoa huduma za afya, tulikaa na kutoa elimu kwa watoa huduma juu ya athari za kuwanyanyapaa wagonjwa hususan wanawake wanapokuja kujifungua na Tunashukuru kumekua na mabadiliko,” amesema Musa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mnuye Kata ya Msimbati Athumani Chande, amesema ushirikishwaji wa Wananchi kwenye miradi hiyo imekua na manufaa sana kwa vijana na imepunguza wimbi la vijana kushiriki katika matukio ya uvunjaji wa amani ikiwemo wizi, ulevi na madawa ya kulevya hivyo kuwa na jamii yenye vijana wanaojitambua.
Aidha, Mtaalam kutoka ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Fransisca Ngwendesha, amewasisitiza wanufaika kuzingatia mila na desturi zenye maadili kwenye Jamii ikiwemo kuondokana na ukatili wa kijinsia na watoto.