Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ilifanya kikao chake cha 229 tarehe 18 Desemba 2023, Fax No. 2234217
kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo wa uchumi. Katika tathmini yake, Kamati ilibaini kuwa utekelezaji wa sera ya fedha, umechangia kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki ndani ya lengo la asilimia 5, kuongeza uzalishaji katika shughuli mbalimbali za kiuchumi pamoja na kudumisha uthabiti wa sekta ya fedha. Utekelezaji huu, ukichagiwa na Sera thabiti ya bajeti na ongezeko la mapato yatokanayo na mauzo ya bidhaa nje ya nchi pamoja na shughuli za utalii umesaidia kupunguza uhaba wa fedha za kigeni nchini kwa mwezi Oktoba na Novemba 2023.
Kamati pia ilitathmini mwenendo wa uchumi wa dunia na kubaini kuwa uchumi wa dunia umeendelea kubaki dhaifu kwa kipindi cha mwaka 2023, kutokana na migogoro ya kisiasa, kubanwa kwa sera ya fedha katika nchi nyingi duniani na ongezeko la bei za nishati. Hata hivyo, hali hii inatarajiwa kuimarika mwaka 2024 kutegemeana na kupungua kwa bei za nishati na matarajio ya kupungua kwa kubanwa kwa sera ya fedha katika nchi zilizoendelea pamoja na utatuzi wa migogoro ya kisiasa duniani. Kamati pia ilifanya tathmini ya kina ya mwenendo wa uchumi wa ndani na kubaini kuwa;
- Licha ya changamoto zinazotokana na mtikisiko wa kiuchumi duniani, mwenendo wa uchumi wa ndani ulikuwa wa kuridhisha mwaka 2023, na unatarajiwa kuimarika zaidi mwaka 2024, kutokana na utekelezaji wa sera zenye lengo la kuchochea uzalishaji nchini pamoja na ongezeko la uwekezaji wa sekta binafsi. Pato la Taifa kwa Tanzania Bara lilikua kwa asilimia 5.4 na asilimia 5.2 kwa robo ya kwanza na ya pili ya 2023, mtawalia. Kutokana na ukuaji huu pamoja na tathmini ya viashiria vya awali vya kiuchumi kwa nusu ya pili ya mwaka 2023, ukuaji uchumi unatarajiwa kuwa juu ya makadirio ya asilimia 5 kwa mwaka 2023. Uchumi wa Zanzibar pia uliendelea kuimarika kutokana na kuongezeka kwa shughuli za utalii na uwekezaji wa sekta binafsi. Kutokana na hayo, ukuaji wa pato la taifa kwa Zanzibar ulikuwa kwa asilimia 5 katika robo ya pili ya mwaka 2023 na unatarajiwa kufikia asilimia 7.1 kwa mwaka 2023.
- Mfumuko wa bei kwa Tanzania Bara umeendelea kubaki chini ya lengo la asilimia 5, kufuatia utekelezaji wa sera madhubuti za fedha, bajeti na za kimfumo. Mfumuko wa bei ulipungua kufikia asilimia 3.2 kwa mwezi Novemba na Oktoba 2023 ukilinganisha na asilimia 3.3 iliyorekodiwa kwa kipindi cha miezi mitatu mfululizo hadi Septemba 2023 kutokana na kupungua kwa bei za chakula nchini. Kwa upande wa Zanzibar, mfumuko wa
1
bei uliendelea kupungua kufikia asilimia 6.5 mwezi Oktoba 2023, kutoka asilimia 7.5 mwezi Septemba 2023 kutokana na kushuka kwa bei za chakula na bidhaa zisizo chakula. Mfumuko wa bei unatarajiwa kubakia chini ya lengo la muda wa kati la asilimia 5 kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
iii. Kufuatia utekelezaji thabiti wa sera ya fedha inayolenga kupunguza ongezeko la ukwasi katika uchumi, ukuaji wa ujazi wa fedha ulipungua mwezi Novemba 2023. Ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) ulikua kwa asilimia 13.8 mwezi Novemba 2023, ukilinganisha na asilimia 14.5 kwa mwezi Septemba 2023. Kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ilipungua kufikia asilimia 18.3 mwezi Novemba 2023 ukilinganisha na asilimia 19.5 mwezi Septemba 2023. Hata hivyo, ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ulikuwa juu ya makadirio ya ukuaji wa asilimia 16.4 kwa kipindi kinachoishia Desemba 2023. Aidha, kuongezeka kwa hamasa ya uwekezaji sambamba na uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara nchini zinategemea kuendelea kuchochea ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi.
Ukusanyaji wa mapato ya Serikali ulikuwa wa kuridhisha, ambapo katika miezi minne ya kwanza ya mwaka 2023/24, makusanyo yalifikia asilimia 96 ya lengo kwa Tanzania Bara, huku matumizi yakiendelea kuendana na mapato. Kwa upande wa Zanzibar, ukusanyaji wa mapato ulishabihiana na malengo yaliyowekwa.
- Nakisi ya urari wa biashara, huduma na uhamisho mali nje ya nchi, iliimarika kidogo kutokana na ongezeko la mapato yatokanayo na mauzo ya bidhaa nje ya nchi pamoja na shughuli za utalii. Kufuatia hali hii, nakisi ya urari wa biashara na uhamisho mali nje ya nchi ilifikia dola milioni 3,265.5 mwezi Oktoba 2023, kutoka dola milioni 4,990.1 kwa
mwaka unaoishia Oktoba 2022. Kwa upande wa Zanzibar, nakisi ya urari wa biashara, huduma na uhamisho mali nje ya nchi iliongezeka kufikia dola milioni 477.7 kutoka dola milioni 362.8, kutokana na kupanda kwa gharama za uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje. Akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kutosha ikiwa ni takriban dola bilioni 5 kwa mwezi Novemba 2023, kiasi kinachotosha kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa kipindi kinachozidi miezi minne. Thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani iliipungua kwa asilimia 7.8 kwa mwaka, hali inayoakisi upungufu wa fedha za kigeni nchini. Hata hivyo, akiba ya fedha za kigeni inatarajiwa kuendelea kuwa ya kutosha.
- Sekta ya fedha iliendelea kuwa thabiti. Sekta ya benki ilibaki imara ikiwa na mitaji ya kutosha na ubora wa rasilimali za benki ukiongezeka, kiwango cha mikopo chechefu kilipungua kufikia asilimia 5.3 mwezi Oktoba 2023, kutoka asilimia 7.2 mwezi Oktoba 2022.
Kamati ya Sera ya fedha iliridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Benki Kuu katika kukabiliana na uhaba wa fedha za kigeni nchini, Vilevile, utekelezaji wa sera zenye lengo la kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi, unatarajiwa kuimarisha
2
urari wa bidhaa, huduma na uhamisho mali nje ya nchi, kuongeza akiba ya fedha za kigeni na hivyo kupelekea utulivu wa thamani ya Shilingi. Kamati pia ilipongeza jitihada zilizochukuliwa na kuwezesha kufikiwa kwa malengo ya programu mbalimbali za kiuchumi nchini ikiwa ni pamoja na yale yaliyoainishwa kwenye programu ya IMF ya Extended Credit Facility (ECF).
Vilevile, Kamati ilibaini na kupongeza hatua zillizofikiwa na Benki Kuu ya Tanzania katika kuhamia kwenye mfumo mpya wa Utekelezaji wa Sera ya Fedha utakaoanza Januari 2024. Utekelezaji huu utalenga riba za muda mfupi katika soko la fedha badala ya fedha taslimu (reserve money) katika kukabiliana na mfumuko wa bei na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi. Mfumo huu unatambulika kama Mfumo wa Utekelezaji wa Sera ya Fedha unaotumia riba.
Kwa kuzingatia matarajio ya utulivu katika mfumuko wa bei na kuendelea kuimarika kwa mazingira ya biashara nchini, Kamati iliridhia kuendelea na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kupunguza ongezeko la ukwasi katika uchumi mwezi Desemba 2023. Maamuzi haya yalizingatia mwenendo usioridhisha katika uchumi wa dunia.
GAVANA
BENKI KUU YA TANZANIA