Na WAF – Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu amewahimiza wabunifu wa Huduma za Afya za Kidigitali kushirikiana na Serikali ili kuweza kuboresha huduma bora za kiafya kwa wananchi kupitia TEHAMA.
Dkt. Jingu ameyasema hayo katika Jukwaa la Wabunifu wa Afya ya Kidijitali lililofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere leo Disemba 18, 2023 lililohudhuriwa na wadau mbalimbali kama vile Mamlaka ya Serikali Mtandao (EGA) na wadau sekta binafsi nchini.
“Tunafahamu kwamba dunia ya sasa ni ya teknolojia na teknolojia za kidigitali. Serikali, kupitia Wizara ya Afya, imeweka mikakati mbalimbali kutumia teknolojia za kisasa katika kuboresha utoaji wa huduma za Afya”. Amesema Dkt. Jingu.
Aidha, Dkt. Jingu amesema Serikali, kupitia Wizara ya Afya, imeongeza kasi ya utoaji wa huduma bora za Afya kwa wananchi kwa kutumia teknolojia za kidigitali. Teknolojia hizi zimeweza kusaidia kutoa huduma bora kwa haraka, ufanisi, kasi na usahihi zitakazoruhusu upatikanaji wa huduma za Afya kwa urahisi.
Pia, Dkt. Jingu amesema Wizara ya Afya imeanzisha Kituo cha Afya cha Kidijitali (CDH) yenye lengo la kuhakikisha wadau wote kwenye sekta ya Afya wanafanya kazi kwa pamoja na wanapata njia wanayoweza kushirikiana katika kutatua changamoto zilizopo katika sekta ya afya ili kuboresha huduma za Afya nchini.
“Teknolojia italeta mapinduzi makubwa, na mapinduzi haya yanawezekana, kama tutaweza kufanya kazi kwa pamoja”. Amesema Dkt. Jingu.