Na.Alex Sonna
YANGA SC wameendelea kugawa dozi mechi za Ligi Kuu ya NBC Tanzania bara baada ya kupata ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Mtibwa Sugar Mchezo uliopigwa uwanja wa Chamazi Complex nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Yanga walienda mapumziko wakiwa mbele kwa bao moja lililofungwa na Kiungo Mshambuliaji Stephane Aziz Ki dakika ya 45 +1 kwa Mkwaju wa Penalti baada ya Clement Mzize kuchezewa rafu ndani ya 18.
Kipindi cha pili Timu zote zilifanya mabadiliko hata hivyo Yanga walinufaika na mabadiliko hayo mnamo dakika ya 65 Stephane Aziz Ki akifunga bao la pili na kuzidi kuongoza msimamo wa wafugaji akiwa na mabao 9 mpaka sasa.
Kennedy Musonda alifunga bao safi la kideoni la tatu dakika 76 na katika dakika ya 83 winga hatari Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ alipigiria msumari wa nne kwa shuti kali na Seif Karihe alifunga bao la kufutia machozi dakika ya 90 +5.
Kwa matokeo hayo Yanga SC imefikisha alama 27 ikiwa imecheza mechi 10 ikisalia nafasi ya pili,nyuma ya Azam FC wenye alama 28 wakiwa wamecheza mechi 12 huku Mtibwa Sugar wanaendelea kuburuza mkia wakiwa na alama 5 baada ya mechi 13.