Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akisalimiana na Mhashamu Baba Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga – Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Tanzania na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
(TEC); kabla ya kufanyika kwa Mahafali ya 26 Chuo hicho, tarehe 16 Desemba 2023 katika Viwanja vya Raila Amoro Odinga jijini Mwanza
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko akisalimiana na Viongozi mbalimbali mara baada ya kuwasili katika Mahafali ya 26 ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino jijini Mwanza leo.
………..
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
amewataka wahitimu wa Vyuo mbalimbali nchini mara baada ya kuajiriwa
au kujiajiri wakasikilize na kuhudumia watu wa makundi yote hasa
maskini kwani kila mwananchi ana haki ya kupata huduma bora bila
kujali hadhi aliyonayo.
Amesema hayo katika Mahafali ya 26 ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu
Augustino cha Tanzania (SAUT), tarehe 16 Desemba 2023 yaliyofanyika
katika Viwanja vya Raila Odinga jijini Mwanza.
“Ndugu Wahitimu na wale ambao tupo makazini, tusikilize watu wa
makundi yote hasa wale wasio na kitu cha kutulipa na tuone fahari ya
kunyanyua hadhi ya watanzania kwenda kwenye maisha yaliyo bora zaidi
kwani ukisaidia maskini unakuwa umesaidia wananchi wengi zaidi.”
Amesema Dkt. Biteko
Aidha, Dkt. Biteko ametaka Wahitimu nchini kuchukia rushwa katika
utoaji wa huduma kwa wananchi na kuwaeleza kuwa, waone fahari kuchukia
rushwa na waichukie kwa kuonekana kwa macho ili kutoa heshima kwa Vyuo
na nchi kwa ujumla.
Dkt. Biteko amesema kuwa, Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri
na wezeshi kwa kila mtu mwenye juhudi na kuhakikisha kwamba mazingira
ya kufanya kazi yanakuwa bora, pia Serikali itaendelea kuweza
mazingira mazuri ya uwekezaji, na kuendelea kuajiri kila itakapopata
nafasi za kuajiri wahitimu wenye taaluma mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuma salam za
pongezi kwa Jumuiya ya wana SAUT na wahitimu kwa Mahafali hayo ya 26.
Amesema kuwa, Rais anaamini kwamba, uwepo wa Taasisi hiyo ya SAUT
inaongeza mchango mkubwa katika mipango ya Serikali katika kusukuma
mbele maendeleo ya nchi kupitia wahitimu wa kada mbalimbali katika
Chuo hicho.
Kwa Wahitimu wote, Dkt. Biteko amewaasa kwamba watoe huduma kwa haki
na waende kujifunza kwa walio makazini kwani kujifunza hakukomi, na
waendelee kupata ujuzi kupitia ngazi nyingine za masomo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa, eneo hilo la Chuo cha
SAUT litawekwa taa za barabarani ili kuongeza usalama kwa wanafunzi
katika Chuo hicho akieleza kuwa Mkandarasi wa kufanya kazi hiyo
ameshapatikana.
Kuhusu barabara katika eneo hilo ambalo alielezwa na viongozi wa Chuo
kuwa si rafiki ameahidi kuwa, Serikali nalichukua suala hilo na
italifanyia kazi.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha SAUT, Profesa Costa Ricky
Mahalu, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Sita, kwa kuvisimamia na
kuviendeleza Vyuo vikuu nchini ambavyo vimeendelea kuzalisha wahitimu
wa kada mbalimbali.
Pia ameshukuru uhusiano mzuri ulipo kati ya Serikali na Chuo hicho
ambao umepelekea kupata wanafunzi wa kutosha kila mwaka katika kada
mbalimbali na mikopo inayotolewa kupitia Bodi ya Mikopo ambayo
inawajumuisha wanafunzi ngazi ya astashahada.
Katika Mahafali hayo Jumla ya wanafunzi 3,066 wamehitimu masomo yao
katika ngazi mbalimbali ikiwemo Shahada ya Uzamivu katika Mawasiliano
ya Umma, Shahada ya Uzamili ya Utawala na Biashara, Shahada ya
Uzamili ya Uchumi na Shahada ya Uzamili ya Sheria.