Waziri wa Wizara ya Ujenzi,Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Dkt. Khalid Salum Mohammed akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mapinduzi ya sekta ya ujenzi mawasilaiano na uchukuzi huko Karume house Mjini Unguja.
Mwandishi wa habari Bahari FM Khadija Juma Iddi akiuliza swali kwa Waziri wa Wizara ya ujenzi ,mawasiliano na uchukuzi Zanzibar Dkt. Khalid Salum Mohammed wakati akielezea kuhusu mapinduzi ya sekta ya ujenzi mawasilaiano na uchukuzi huko Karume house Mjini Unguja.
PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR
Na Sabiha Khamis , Maelezo Zanzibar
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe. Khalid Salum Mohamed amesema Serikali ya awamu ya nane imeleta mageuzi makubwa katika sekta za wizara hiyo na kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya sekta hiyo kuelekea kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar Waziri huyo amesema Wizara imefanikiwa kuimarisha miundombinu mbali mbali ili kuweka mazingira rafiki kwa wananchi wake.
Akizungumzia Sekta ya usafiri ardhini amesema Serikali inaendelea na juhudi za ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa kujenga barabara zenye viwango vinavyostahili na kuweka taa za barabarani na njia za wanaotembea kwa miguu pamoja na barabara za juu (fly over) ili kuweka haiba nzuri ya Nchi.
“Zanzibar kwa mara ya kwanza inajenga barabara za juu (fly over) ili kupunguza msongamano wa magari wakati wa asubuhi wananchi wanapokwenda kwenye shughuli zao za kutafuta riziki na jioni wanaporudi majumbani kwako” alisema Waziri.
Kuhusu suala na mawasiliano Dk. Khalid alisema Serikali imefanikiwa kujenga zaidi ya vituo 10 vya Tehama katika kila wilaya pamoja na kuwa na mpango wa kuongeza mkonga mwengine wa mawasiliano ambao utatoka Mombasa kupitia Micheweni Pemba hadi kufikia Fumba ili kupata huduma za mawasiliano kwa urahisi zaidi.
Alisema Wizara inatarajia kuazisha vituo vya kuhifadhi data Fumba na Micheweni hivyo amezitaka mamlaka husika kuwaanda vipaji vya ubunifu wa kuandaa mfumo wa mawasiliano ili kuifikisha nchi katika matumizi ya teknolojia ya mawasiliano.
Katika suala la maendeleo ya usafiri wa baharini alisema Serikali imefanikiwa kuimarisha bandari ya Mkoani kwa kuweka njia ya abiria wanaotembea kwa miguu kwa usalama wa abiria hao na mali zao.
Aidha alisema Serikali ina mpango wa kujenga eneo la kupumzikia katika bandari hiyo pamoja na kuzimarisha bandari za Pemba ikiweo Wete,Mkoani na Shumba ili kuiinua pemba kiuchumi.
Hafla hiyo ikiwa ni muendelezo wa mkutano wa Mawaziri na waandishi wa habari kuelezea utekelezaji, maendeleo na mafanikio ya Wizara zao kuelekea miaka 60 ya mapinduzi ya Zanzibar.