Na Gideon Gregory, Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju ameielekeza Ofisi ya Rais TAMISEMI kuhakikisha mpango wa Taifa wa Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) unasainiwa ndani ya wiki hii na wiki ijayo unaenda katika mikoa na Halmashauri zote nchini kwaajili ya utelezaji.
Mpanju ametoa maelekezo hayoJijini Dodoma Disemba 13,2023 wakati akifunga mkutano wa siku tatu wa Kitaifa wa Wadau wa mpango wa sekta zote ambapo kiliambatana na uzinduzi wa Mwongozo Jumuishi wa Taifa wa Utekelezaji wa Mpango huo siku ya kwanza.
“Wadau wako tayari kuunga mkono, yaani ifikapo Ijumaa ya wiki ijayo ziwe zimeenda ili wadau hawa wakose kisingizio waende waende wakatekeleze na maafisa Mipango na uratibu wakasimamie uingizwaji wa bajeti kwenye bajeti ya 2024/25 kwasababu michakato imekwisha kuanza,”amesema Mpanju.
Sambamba na hilo Mpanju amesema kuwa kupitia Wizara hiyo Serikali imetoa rai kwa watekelezaji wa mpango huo kuhakikisha wanasimamia vyema mipango yote waliojiwekea inatekelezeka kikamilifu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya mtoto kutoka wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Sebastian Kitiku amesema kuwa lengo kuu la kuandaa mpango utakao wawezesha wajumbe kutoka ngazi ya mkoa kwenda kuingiza mpango katika bajeti ya serikali kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25.
“Niwashukuru sana wenzetu makatibu tawala kutoka ngazi za mikoa ambao kwakweli wamekuwa msaada mkubwa katika kuandaa mipango na nia walio hionesha katika kwenda kuingiza hayo majukumu kwenye mipango ya ngazi ya mikoa na Halmashauri,”amesema.
Naye Mkurugenzi Mkazi wa Children in Crossfire, Craig Ferla amesema programu hiyo kwa kiwango kikubwa inabeba dira na mustakabari wa maisha ya watoto ikizingatiwa na robo ya watanzania ni watoto chini ya miaka minane.
“Programu hii kwa kiwango kikubwa inabeba maono makuu ya taifa letu, naamini fika watoto wetu wako kwenye mikono salama na kila mkono humu ndani ukijitoa muhanga kwa mustakabari bora wa watoto wetu na mipango kazi inatoa matumaini zaidi kwenye pembe zote za nchi na kuna juhudi za makusudi kuhakikisha bajeti iliyo jikoni inawabeba zaidi watoto wetu,”amesema.