Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nandagala A wilayani Ruangwa wakichota maji katika moja ya vituo maalum vya kuchotea maji vilivyojengwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijiji(Ruwasa)wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.
Tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 150,000 za maji lililojengwa katika mradi wa maji Nandagala linalohudumia wakazi wa vijiji vya Nandagala A na B wilayani Ruangwa.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi Mhandisi Lawrence Mapunda kulia,akizungumza na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Muhulu wilayani humo kuhusu umuhimu wa kutunza miradi ya maji inayotekelezwa na serikali ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Na Muhidin Amri
Ruangwa
ZAIDI ya Wakazi 7,000 wa vijiji vya Nandagala A na B katika jimbo la Ruangwa wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi,wameondokana na kero ya upatikanaji wa maji safi na salama baada ya wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji ya bomba wa Nandagala kwa gharama ya Sh.bilioni 1.6.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Ruangwa Mhandisi Lawrence Mapunda alisema,mradi huo ulianza kutekelezwa mwezi Oktoba mwaka jana na kwa sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 98 na umeanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi wa vijiji hivyo.
Kwa mujibu wa Mapunda ni kwamba,awali wakazi hao walikuwa wanakwenda kuchota maji kwenye visima walivyochimbwa kwa mikono na wengine kutumia maji ya mito hasa wakati wa masika ambayo hayakuwa safi na salama.
Alitaja chanzo cha mradi ni visima viwili vilivyochimbwa katika eneo la Namahema A chenye uwezo wa kuzalisha lita 18,000 kwa saa na kisima kingine kilichopo katika kijiji cha Namahema B chenye uwezo wa kuzalisha lita 4,500 kwa saa.
Mapunda alieleza kuwa,kisima cha Namahema B kinapeleka maji kwenye tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 50,000 na linahudumia taasisi mbalimbali za serikali ikiwemo Shule ya Sekondari ya Mary Majaliwa, chuo cha ufundi(Veta)kituo cha Afya na shule ya msingi Nandagala A.
Alisema,kisima cha Namahema B maji yake yanapelekwa kwenye tenki la ujazo wa lita 200,000 na maji yake yanapelekwa moja kwa moja kwa wananchi wa vijiji vya Nandagala A na B kupitia vituo maalum vya kuchotea maji.
Aidha alisema,Ruwasa wilayani Ruangwa imekamilisha ujenzi wa mradi wa maji Namichiga unaohudumia vijiji vya Chibula,Namichiga A,Namichiga B na Mulu vyenye wakazi 7,500 kwa gharama ya Sh.bilioni 1.5.
Alisema,kabla mradi huo wananchi wa vijiji hivyo walikuwa kwenye mateso makubwa ya kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi yao kwenye visima vya asili vinavyofanya kazi wakati wa masika na inapofika muda wa kiangazi vinakauka.
Pia alisema,wametekeleza miradi mingine miwili ikiwemo wa Nanganga unaohudumia vijiji vinne,na mradi wa Liugulu unaohudumia vijiji viwili na miradi hiyo imekamilika kwa zaidi ya asilimia 98.
Mapunda amewatoa hofu wananchi kwa kueleza kuwa,maji yanayotolewa na Ruwasa wilayani humo ni safi na salama na yana ubora mkubwa na yamethibitishwa na shirika la viwango nchini(TBS) na shirika la afya Duniani(WHO).
Katibu wa chombo cha watumia huduma ya maji ngazi ya jamii(CBWSO) kata ya Namichiga (Chimuna) Omari Nikapa alisema,mradi huo ni msaada mkubwa kwa wananchi kwani umewasaidia sana kupata huduma ya maji safi na salama kwenye makazi yao.
Aidha alisema,tangu chombo kilipoanzishwa mwezi Septemba mwaka huu wamefanikiwa kukusanya jumla ya Sh.milioni 7 na kwa mwezi wanakusanya Sh.milioni 3 zinazotokana na mauzo ya maji kwa wananchi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Muhulu Bakari Mohamed,ameipongeza Serikali na wataalam wa Ruwasa wilaya ya Ruangwa kwa kutekeleza mradi huo ambao umemaliza kero na kuboresha huduma ya maji.
Alisema kabla ya mradi huo,wananchi wa kijiji cha Muhulu hasa akina mama walikuwa kwenye migogoro ya mara kwa mara inayotokana na kugombea maji wanapofika kwenye visima vya asili na wengine kuachika na waume zao wanapochelewa kurudi nyumbani kutoka kutafuta maji kwa matumizi ya familia.
Mkazi wa kijiji cha Nandagala A Salma Nahenje alisema,awali walikaa zaidi ya siku tatu bila kuoga kutokana na uhaba wa maji kwenye kijiji hicho kwa kuwa maji waliyobahatika kuyapata yalitumika kwa mambo muhimu kwa ajili ya kupikia chakula na kunywa.