Afisa Forodha Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw. Donald akiwasilisha mada kwa Wajasiriamali katika Maonesho ya Nguvu Kazi/Jua Kali yanayofanyika katika viwanja vya Cercle Hyppique (Golf Course), jiji la Bujumbura, nchini Burundi.
Baadhi ya Wajasiriamali kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa katika kongamano kwenye Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu Nguvu Kazi/Jua Kali yanayofanyika jiji la Bujumbura, nchini Burundi.
Na; Mwandishi Wetu – Bujumbura, BURUNDI
Wajasiriamali Wadogo na wa Kati kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wametakiwa kuchangamkia fursa za Soko Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).
Rai hiyo imetolewa na Afisa Forodha Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw. Donald Tindamanyire wakati akiwasilisha mada kuhusu “Umuhimu wa Kuwandaa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati Kuchangamkia Fusa za Soko Huru la Biashara kwa Wajasiriama” kwenye maadhimisho ya “SIKU YA TANZANIA” yaliyofanyika jijini Bujumbura tarehe 10 Desemba 2023 kwenye maonesho ya Nguvu Kazi/Jua Kali.
Bw. Tindamanyire amesema kuwa wajasiriamali wana nafasi kubwa katika kutumia soko hilo la Afrika na kueleza kuwa kinachohitajika sasa ni wajasiriamali hao kujifunza taratibu mbalimbali zinazohitajika kwenye kulifikia soko hilo zikiwemo sheria, taratibu na kanuni za ufanyaji biashara za kuvuka mipaka ili kuepuka vikwazo vinavyoweza kujitokeza pindi wanapohitaji kutumia soko hilo.
Vile vile, amewashauri wajasiriamali kuboresha na kuongeza thamani ya bidhaa zao pamoja na kutumia teknolojia ili kuzalisha kwa wingi na kuweza kuingia kwenye ushindani na nchi zingine za Afrika.
Pia Bw. Tindamanyire alitumia fursa hiyo kuwahimiza wanawake na vijana kutumia fursa ya soko hilo ambalo limeandaa Itifaki mahsusi kwa ajili ya kundi hayo.
Itifaki ya Soko Huru la Biashara Barani Afrika hadi sasa imeridhiwa na nchi 47 kati ya 54 za Afrika ikiwemo Tanzania na imeanza kutumika tangu mwezi Januari 2021.