Na Gideon Gregory, Dodoma.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa rai kwa watekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) kuhakikisha wanatenga bajeti ili kufanikisha malengo ya mpango huo.
Waziri Dkt. Gwajima metoa rai hiyo leo Desemba 11,2023 Jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Kitaifa wa Wadau wa mpango wa sekta zote sambamba na kuzindua Mwongozo Jumuishi wa Taifa wa Utekelezaji wa Mpango huo.
Aidha ameyahimiza Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuongeza jitihada ya kuwekeza katika program hiyo kwa kushirikiana na Serikali katika ngazi zote na kuwasisitiza Waandishi wa habari Vinara kupitia umoja wao kuendelea kuelimisha jamii kuhusu program ya MMMAM na tija yake kwa watoto.
“Naomba nitumie fursa hii niwahimize pia Wadau kushiriki vema katika mkutano wa Wadau wa MMMAM wa Afrika Mashariki utakaofanyika Jijini Dar es Salaam, Machi 2024,”amesema.
Amesema katika kipindi cha miaka miwili tangu kuzinduliwa kwa mpango huo, mafanikio yanaonekana katika utekelezaji wake ikiwemo programu kutekelezwa kwenye Halmashauri 70 za Mikoa 10 ya awamu ya kwanza na mpango wa kukamilisha Programu kwa Halmashauri zote 184 utafikiwa Aprili, 2024.
Sanjari na hayo ameongeza kuwa, Wizara inatambua umuhimu wa Wadau hao katika utekelezaji wa PJT MMMAM ambapo amewataka kuainisha vipaumbele kwa uratibu wa Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa ili kuingizwa kwenye bajeti ya Serikali ya 2024/25 kwani kwa kufanya hivyo, uwekezaji wa malezi na makuzi ya watoto wa miaka 0-8 utaongezeka.
“Hakikisheni mnafanya kazi kama timu kwa kuratibiana vizuri kwa kuwa malengo ya programu ya MMMAM hayawezi kufikiwa bila kuzishirikisha sekta zote kwa uwiano na umuhimu unaofanana “alisema Dkt Gwajima.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari UTPC Kenneth Simbaya amebainisha kuwa kupitia Klabu hizo pamoja na vinara wanaungana na Wadau na Serikali kutekeleza mpango huo.
“Nikuhakikishie mhe. Waziri kuwa tunaungana nanyi katika kuhakiksha mpango huu unatimia na utekelezwa kadri ambavyo imekusudiwa na kuleta tija kwani tumekuwa tukishirikiana nanyi vyema,”amesema.