Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Bi.Jenifa Omolo akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha Dkt.Mwigulu Nchemba kwenye Duru ya pili ya sherehe za mahafali ya 37 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini yaliyofanyika katika Kituo cha mafunzo cha Kanda ya ziwa Jijini Mwanza
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la uongozi wa Chuo Dkt.Samwel Werema akizungumza kwenye mahafali ya 37 ya Chuo Duru ya pili yaliyofanyika katika Kituo cha mafunzo cha Kanda ya ziwa Mwanza.
Wahitimu wakiwa kwenye sherehe za mahafali ya 37 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini yaliyofanyika katika Kituo cha mafunzo cha Kanda ya ziwa Jijini Mwanza.
Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Profesa Hozen Mayaya akizungumza kwenye Duru ya pili ya sherehe za mahafali ya 37 ya Chuo yaliyofanyika katika Kituo cha mafunzo cha Kanda ya ziwa Mwanza.
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wahitimu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Kituo Cha mafunzo cha Kanda ya ziwa Mwanza wameaswa kujihadhari na ugonjwa wa ukimwi hatua itakayosaidia kutimiza ndoto zao zaidi.
Rai hiyo ilitolewa Jana Desemba 8, 2023 na Katibu Mkuu wa Wizara ya fedha Bi.Jenifa Omolo kwa niaba ya Waziri wa Fedha Dkt.Mwigulu Nchemba kwenye Duru ya pili ya sherehe za mahafali ya 37 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini yaliyofanyika katika Kituo Cha mafunzo cha Kanda ya ziwa Jijini Mwanza.
Omolo amesema ugonjwa huo bado upo na takwimu zinaonesha waathirika zaidi ni vijana kati ya miaka 15 hadi 24 umri ambao ni sehemu ya nguvu kazi ya Taifa.
“Ninawasihi endeleeni kuchukua tahadhari zote ili kujiepusha na ugonjwa huo,kumbukeni mnategemewa siyo tu na wazazi wenu bali na jamii nzima na Taifa kwa ujumla,nyie ndio nguvu kazi ya kuiwezesha nchi kupanda kiuchumi kutoka hapa tulipo kwenda uchumi wa juu zaidi kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi”, amesema Omolo
Amesema watanzania wanapaswa kubadili fikra na mtazamo juu ya janga la Ukimwi kwa kuongeza nguvu katika eneo la kuzuia maambukizi mapya ya VVU hasa kwa vijana.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha mafunzo cha Kanda ya ziwa Profesa Juvenal Nkonoki, amesema wahitimu 2,618 wametunukiwa tuzo mbalimbali baada ya safari ndefu na ngumu ya kuitafuta elimu kati yao wanaume ni 1,211 na wanawake 1,407.
Amesema katika kuwajengea wanafunzi umahiri Kituo kiliwapeleka kwenye mafunzo ya vitendo wanafunzi wa Astashahada katika vijiji vya Nasa Jineri,Mwanangi,Yitimbwa na Nyambiti ‘B’ ambapo walitengeneza mpango wa maendeleo ya Kijiji.
Naye Mkuu wa Chuo hicho Profesa Hozen Mayaya, amesema sherehe hizo za mahafali zimefayika kipindi ambacho wamefunga rasmi historia ya kutoa huduma kwenye majengo ya kupanga na sasa wapo kwenye majengo yao jambo ambalo awali lilionekana ni gumu.
“Katika ujenzi wa miundombinu tumeendelea kupokea kwa wakati fedha za maendeleo kwaajili ya miradi ya Maendeleo inayojengwa kwa kasi katika taasisi yetu,kila tunapowasilisha certificate kwaajili ya malipo Wizara imekuwa ikitoa fedha kwa wakati hali hii imetutia moyo sana”, amesema Profesa Mayaya
Dkt.Samweli Werema ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la uongozi wa Chuo, amesema ndani ya mwaka mmoja chuo hicho kimepata mafaniko mengi ikiwemo kushika nafasi ya kwanza ya utendaji bora katika usimamizi wa rasilimali watu na Utawala bora kwa vyuo vya kati na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini pamoja na kuendelea kupata hati safi ya mahesabu ya Chuo kutokana na uzingativu wa kanuni za fedha na miongozo mbalimbali ya Serikali katika ukusanyaji na matumizi ya fedha za imma.