Na Alex Sonna, Dodoma
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeteketeza bidhaa za chakula na vipodozi visivyokuwa na ubora kilo 837,075.07 zenye thamani ya zaidi ya Sh. Milioni 21.8 zilizokamatwa kutoka kwenye maeneo ya biashara kwenye Mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora.
Bidhaa hizo zimeteketezwa mwishoni mwa wiki katika dampo la Chidaya jijini Dodoma baada ya kukamatwa kwenye ukaguzi uliofanyika kwenye maeneo tajwa kati ya Aprili hadi Novemba, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuteketeza bidhaa hizo, Ofisa Udhibiti Ubora wa TBS Kanda ya Kati,Bw. Vicent Tarimo, alisema bidhaa zilizoteketezwa zinahusisha zilizoisha muda wake wa matumizi, zenye viambata sumu na zile ambazo tarehe ya mwisho wa matumizi zimeharishwa baada ya kuhaririwa.
Kuahirishwa kwa tarehe ya mwisho ya mutumizi ya bidhaa husika kumekuwa kukifanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu.
Kwa mujibu wa Tarimo madhara uwepo wa bidhaa zilizoisha muda wa matumizi na zenye viambato sumu ni kuathiri uchumi wa nchi pamoja na afya za watumiaji bidhaa za chakula zilizoisha muda wa matumizi na zile ambazo tarehe za mwisho wa matumizi zimehaririwa zinaathiri upatikanaji wa virutubisho vinavyotegemewa.
“Bidhaa hizi zinaweza kusababisha magonjwa ya muda mfupi na mrefu ikiwemo saratani,” alisema Tarimo.
Kadhalika, alisema katika bidhaa zenye viambata vya sumu athari zake za muda mfupi na mrefu ni pamoja na kuathiri ngozi, macho, mfumo wa uzazi kwa akina mama, ukuaji kwa watoto na magonjwa ya saratani hasa ya ngozi.
“Ukaguzi ni endelevu kwa mikoa yote nchini na wito wangu kwa wafanyabiashara kukagua bidhaa zao mara kwa mara kujiridhisha na ubora wake,” alisema.
Aidha, aliwataka kutunza bidhaa hizo kwa mujibu wa taratibu za wazalishaji,kuepuka kuuza bidhaa za vipodozi zenye viambato sumu na kuacha mara moja kuhariri taarifa za mwisho wa matumizi.
Alionya kuwa kali za kisheria zinaendelea kuchukuliwa kwa wafanyabishara wasio waaminifu kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zake.